TAASISI ZA BIMA ZITOE ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU UMUHIMU WA KUKATA BIMA

 

Muhtasari: Taasisi za Bima nchini zimeshauriwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kukata bima kwenye shughuli wanazofanya  kwa wananchi ambao inadaiwa wengi wao hawana uelewa wa huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA ya usimamizi wa bima nchini (TIRA) kwa kushirikiana na wadau wa bima wameshauriwa kutoa elimu ya bima kwa wananchi hasa yanapotokea majanga kwa wateja wao ili wananchi wengi wajue umuhimu wa kukatia bima shughuli zao za uchumi.

Ushauri huo umetolewa leo ijumaa, Septemba 13, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, kwenye matembezi ya kuadhimisha siku ya bima nchini yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

Mayanja amesema ni Watanzania wachache wenye uelewa kuhusu huduma za bima na kundi kubwa halina elimu hivyo yanapotokea majanga kwa wateja wao wenye bima basi watumie fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima.


Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, Janeth Mayanja


“Nina fahamu Tira mnafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi lakini ukiangalia namna nchi yetu na wananchi wake wanavyopiga hatua za kimaendeleo kwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi bado kuna changamoto za wadau kukatia bima shughuli wanazozifanya japo tumeona ni kwa jinsi gani bima imeweza kujerejesha kile ambacho kimepotea,” amesema Mayanja

Amezitaka taasisi za bima nchini ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha Watanzania walio wengi wanapata elimu ya bima ambapo wakipata elimu ya kutosha kwa fursa zilizopo watachukua hatua maana wenye uelewa wa bima ni wale tu ambao wapo kwenye nafasi mbalimbali za utumishi au wafanyabiashara wakubwa huku kundi kubwa la wananchi wakiachwa nyuma.

“Lakini kuna kundi kubwa sana ambao hawafahamu wala hawana uelewa mkubwa juu ya bidhaa za bima mlizonazo kwa hiyo niwaombe tuongeze nguvu katika eneo hilo ili tuwe na maendeleo ya pamoja,” amesema Mayanja na kuongeza kuwa.

“Najua yanapotokea majanga mbalimbali mmekuwa mkirejesha mitaji ya shughuli zile ambazo zimepotea basi ikitokea wakati huo fanyeni promo ya kutosha ili watanzania wajue ya kwamba yanawezekana kwa sababu msipofanya hivyo wataona ni mambo ya kawaida.”


Baadhi ya wadau wa bima wakiwa kwenye matembezi katika kuadhimisha siku ya bima nchini, Jijini Dodoma


Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) Tanzania, Magreth Kongo amesema suala la bima ni la kila Mtanzania kwa sababu kila mwananchi anahitaji huduma za bima ili aweze kupata msaada anapopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo ajali, magonjwa na hata kwenye majanga ya moto

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya kati, Janeth Shango amewataka Watanzania kukatia shughuli zao za kiuchumi bima ili yanapotokea majanga wasitetereke bali waweze kuinuka na kuendelea na mapambano kwa sababu bima inawasaidia wafanyabiashara kurejesha mitaji yao hata baada ya kupata majanga.

“Tunaona mara nyingi masoko yanashika moto na kuteketeza mali zote lakini kama umekatia biashara yako bima baada ya muda unarudi kuendelea na biashara yako tofauti na yule asiye na bima ambapo hupoteza kila kitu na kulazimika kuanza upya,” amesema Shango.

Aidha taasisi hizo za bima nchini zimetoa msaada wa kuchangia damu kwenye kituo cha damu salama kilichopo mkoa wa Dodoma na msaada wa vifaa tiba  vyenye thamani ya Sh15 milioni kwenye wodi ya watoto njiti iliyopo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Mwisho….

 

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI