CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

Muhtasari: Wafanyakazi wa majumbani wameitaka serikali kuridhia  mkataba namba 189 wa Shirika la kazi Duniani (ILO) ili kada hiyo iweze kutambulika kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine nchini.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAFANYAKAZI wa majumbani wameiomba serikali kuridhia mkataba namba 189 wa Shirika la kazi Duniani (ILO) kuhusu  kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani ili waweze kupata haki zao kama wafanyakazi wengine ikiwemo likizo, kujiunga na mifuko ya hifadhi za jamii na kulipwa kima cha chini cha mshahara.

Kauli hiyo imetolewa leo jumanne na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Light for Domestic Workers (LDW) ambayo inajishughulisha na kutoa elimu kuhusu wafanyakazi wa majumbani kujua haki na majukumu yao, Beatrice Johnson wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama cha wafanyakazi wa mahotelini na majumbani (Chodawu) Jijini Dodoma.

Beatrice amesema wafanyakazi wa majumbani wanapitia changamoto nyingi kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuwa hakuna sheria inayowalinda kwani waajiri wengi huwachukulia kama ndugu na kuwalipa malipo kidogo huku wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya light for domestic workers Beatrice Johnson akizungumza kuhusu mkataba namba 189 wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani


“Tunaiomba serikali iridhie mkataba namba 189 wa shirika la kazi duniani (ILO) ili wafanyakazi wa majumbani waweze kutambulika kama wafanyakazi wengine nchini kwani pamoja na majukumu makubwa waliyonayo ya kutunza familia na kulea watoto lakini hawatambuliki wala kuthaminiwa kama wafanyakazi wengine,”amesema Beatrice na kuongeza kuwa,

“Mojawapo ya changamoto wanazopitia wafanyakazi wa majumbani ni pamoja na malipo kidogo pamoja na majukumu makubwa ambayo wanayafanya kwani wengine hulipwa mshahara kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 na wakati serikali ilishatangaza kima cha chini cha mshahara wetu ni Sh60,000 kwa anayekaa hapo hapo na kwa yule anayekwenda na kurudi ni Sh120,000.”

Amewaomba pia wabunge wapitishe sheria hiyo kwenye kikao cha Bunge la mwezi Septemba mwaka huu ili sasa kazi za majumbani zitambulike kama kazi za staha.

Amesema pamoja na serikali kuitambua kada ya wafanyakazi wa majumbani lakini maofisa wa kazi hawana mamlaka ya kukagua nyumba ya mtu binafsi kama eneo la kazi na ndiyo maana wafanyakazi wengi wa majumbani wanateseka kwenye nyumba wanazofanya kazi bila hata viongozi wa serikali za mitaa kujua.

Amesema mkataba huo una mambo mengi mazuri ikiwemo kutambulika kwa wafanyakazi wa majumbani na viongozi wa eneo analofanyia kazi ili hata akipata changamoto yoyote ajue mahali pa kuripoti tofauti na sasa ambapo wafanyakazi wanatolewa mbali na kufungiwa ndani bila kujulikana hivyo hata wakipata changamoto wanakuwa hawajui pa kuripoti.



Kamishna msaidizi wa kazi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kazi vijana ajira na watu wenye ulemavu, Andrew Mwalwisi akizungumza kwenye mkutano mkuu wa wafanyakazi wa majumbani ulioandaliwa na chama cha wafanyakazi wa majumbani (Chodawu) Jijini Dodoma


Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu, Andrew Mwalwisi amesema kamishna wa kazi ameshamaliza kufanya kazi yake ya mapitio ya sheria hiyo na ameshaikabidhi kwa waziri mwenye dhamana ya kazi ili aiwasilishe kwenye baraza la mawaziri kabla ya kupelekwa Bungeni.

Mwalwisi amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi wa majumbani na kwamba iko tayari kutetea maslahi yao ikiwemo na wafanyakazi wengine nchini kama vile, madereva wanaoendesha magari ya watu binafsi, wafanyakazi wanaouza maduka, wanaolea wazee, watoto, watu wenye ulemavu na wafanyakazi wanaojitolea kwenye jamii.

“Kabla ya kuruhusu mkataba huu uanze kutumika nchini tulijiridhishe kwanza kwenye mambo mbalimbali yaliyotajwa kwenye mkataba huo kama hajakinzani na sheria zetu za kazi lakini sasa niwahakikishie kuwa tumeshakamilisha kuupitia huo mkataba na sasa tumeukabidhi kwa waziri mwenye dhamana na kazi ili aupeleke kwenye baraza la mawaziri kabla ya kupelekwa Bungeni,” amesema Mwalwisi.

Amesema jamii inapaswa kupewa elimu ya kutosha kabla ya kuridhiwa kwa mkataba huo kwani kama haitaelewa hata kama serikali itaridhia na kusaini mkataba huo hakutakuwa na matokeo mazuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kutetea haki za wafanyakazi wa majumbani (CVM) Tanzania, Magesa Nathanaeli amesema ili wafanyakazi wa majumbani waweze kufanyakazi zao kwa ufasaha wameingia ubia na chuo cha Veta nchini ili kutoa mafunzo kwa wafanyakazi hao kwenye kada ya usafi, mapishi na kutunza watoto na wazee.



Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa wafanyakazi wa majumbani uliofanyika Jijini Dodoma


Amesema kwa sasa nchi za nje hasa Uarabuni wanahitaji wafanyakazi ambao watawasaidia kwenye malezi ya watoto na kuwatunza wazee hivyo wameona soko hilo na kutoa fursa kwa vijana wanaotaka kwenda kufanyakazi nje ya nchi kupata mafunzo kabla ya kwenda huko.

“Tumeona wafanyakazi wengi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi hasa Uarabuni hawana mafunzo ya namna ya kulea watoto pamoja na kuwatunza wazee kazi ambayo ndiyo inahitajika zaidi huko hivyo na sisi tumeiona hii fursa na kuungana na Veta ambao wameanza kutoa mafunzo hayo kwa vijana kabla ya kwenda kuanza kazi,” amesema Nathanael.

Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI