NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA
Muhtasari: Mamlaka ya mapato nchini (TRA) imezindua kitabu cha mwongozo wa kulipa kodi kwa asasi za kiraia zinazotokana na fedha wazopata kwa ajili ya miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ili kupunguza malalamiko ya kodi zinazokatwa kwenye fedha za miradi inayotekelezwa na asasi za kiraia nchini (NGOs) mamlaka ya mapato nchini (TRA) imezindua kitabu cha mwongozo wa kulipa kodi kwa asasi hizo.
Kitabu hicho kimezinduliwa na Kamishna wa kodi za ndani, Alfred Mregi kwa kushirikiana na mtandao wa utetezi wa haki za binadamu (THRDC) Jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema bado kuna faini na riba ambazo huwa zinatozwa na TRA hata kama asasi inakuwa haina mradi unaotekelezwa kwa sababu tu imeshaingizwa kwenye mfumo wa kulipa kodi.
Amesema hiyo huwa inasababisha asasi kuwa na madeni makubwa ya kodi pale wanapopata miradi kwani huwa inaonyesha kuwa hawalipi kodi wakati kodi zao huwa zinatokana na fedha za miradi zinazoingia kwenye akaunti zao za benki.
"Kwa mfano unakuta asasi haijapata mradi kwa miaka mitatu mfululizo lakini kule TRA riba na faini zinaendelea kusoma matokeo yake asasi zinakuwa na madeni makubwa ya kodi asiyolipika na hivyo kurudisha nyuma malengo yao ya kuhudumia jamii," amesema Ole Ngurumwa.
Amesema asasi hizo zina mchango mkubwa kwa jamii kwani zinachangia asilimia 40 ya huduma kwenye sekta ya elimu huku kwenye sekta ya afya zikichangia asilimia 50 na kwenye sekta nyingine kama maji, miundombinu, kilimo na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Kamishna wa kodi za ndani, Alfred Mregi amesema kitabu hicho kimeainisha Kodi zote ambazo zinatakiwa kulipwa na asasi za kiraia kupitia mapato yao ya kila siku.
Amesema kuhusu kuongezeka kwa riba na faini kwenye asasi hizo hilo pia linefanyiwa kazi na kama kuna asasi ambayo ina sababu ya msingi ya kufuatiwa riba hizo inatakiwa iandike barua ya kuomba isamehewe.
Amesema kulipa kodi ni takwa la kisheria hivyo ni lazima walipe kodi kupitia fedha zao za miradi ili nchi iweze kusonga mbele.
"Na kwa sababu inajulikana kuwa mapato yenu ya atoka a na ufadhili wa fedha zinazopitia kwenye akaunti zenu za benki itajulikana tu kwa sababu akaunti itaonyesha hakuna fedha iliyoingia hivyo utasamehewa hizo riba na faini ya kukwepa kulipa kodi lakini kama itaonyesha kuna fedha zilizoingia halafu unaomba msamaha hiyo haitawezekana," amesema Mregi.
Naye mjumbe wa Baraza la Taifa la Asasi za kiraia (NaCongo), Penina Manyanki amesema kitabu hicho kinekuja wakati muafaka kwani hata wale ambao hawajasomea sheria wataweza kuelewa kodi zinazotakiwa kulipwa badala ya kuwatafuta wanasheria wawatafsirie sheria hizo.
Amesema kitabu hicho kitaondoa malalamiko ya asasi za kiraia kwani wengi walikuwa hawajui kodi wanazotakiwa kulipa na mwisho wa siku walikuwa wanajikuta wana madeni makubwa ya kodi ambazo walikuwa hawajui yanatoka wapi.


Comments
Post a Comment