TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI
Muhtasari: Mamlaka
ya dawa na vifaa tiba (TMDA) Kanda ya kati imetoa msaada wa vifaa tiba, dawa na
vitendanishi vyenye thamani ya Sh24 milion kwenye gereza kuu la Isanga lililoko
Mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa, mahabusu na askari magereza
wapatao 1,489.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
WAMILIKI wa maduka ya dawa nchini wametakiwa kufuata masharti ya leseni zao za
kufanya biashara hiyo ili wasihatarishe afya za watumiaji.
Kauli hiyo
imetolewa leo jumanne Juni 18, 2024 na Meneja wa Mamlaka ya dawa na vifaa tiba
(TMDA) kanda ya kati, Sonia Mkumbwa wakati akitoa msaada wa dawa, vifaa tiba na
vitendanishi vyenye thamani ya Sh24 milion kwenye gereza kuu la Isanga lililopo
Mkoani Dodoma.
Mkumbwa
amesema dawa hizo zimepatikana kwenye msako unaofanywa na mamlaka hiyo kwenye
maduka ya dawa na vitendanishi ambavyo vimekuwa vikihifadhiwa kwenye maeneo
ambayo hayapaswi kuhifadhiwa.
Amesema zipo
taratibu na masharti ya kuhifadhi dawa hizo hivyo ni lazima wanaotoa huduma za
dawa za binadamu kuzifuata ili dawa ziendelee kuwa kwenye hali nzuri bila
kuleta madhara kwa binadamu.
“Kikawaida kila dawa ina mazingira yake ya kuhifadhiwa na
dawa nyingi zinatakiwa kuhifadhiwa kwenye nyuzi joto lisilozidi 30 na nyingine
zinatakiwa kuhifadhiwa kwenye majokofu lakini dawa hizo zilikutwa zimehifadhiwa
kwenye mazingira ambayo siyo salama na kama zingeachwa zingeweza kuleta madhara
kwa mtumiaji,” amesema Mkumbwa na kuongeza kuwa
“Kuna dawa
nyingine tumezikuta kwenye maduka ya dawa lakini maduka hayo hayana wataalam wa
kuzitumia dawa hizo hivyo kuleta hatari kwa watumiaji kwa sababu hakuna mtaalam
wa kuwaelekeza matumizi ya dawa hizo hivyo ni lazima wafuate masharti ya leseni
zao ili wasihatarishe maisha ya wagonjwa.”
Dawa ambazo
zimepelekwa kwenye gereza hilo ni pamoja na dawa za kupunguza maumivu, anti bayotiki
dawa za shinikizo la damu na zingine za vidonda ambapo meneja huyo amesema dawa
hizo bado zipo kwenye hali nzuri kwa ajili ya matumizi ya binadamu na hivyo
zinaweza kutumika bila shida yoyote.
Mkuu wa
gereza la Isanga, Zefania Neligwa amesema msaada huo umekuja kwa wakati kwani
gereza hilo linapokea watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya huku wengine
wakija na majeraha makubwa yanayohitaji matibabu ya kina.
Amesema hadi
leo gereza hilo lina jumla ya wafungwa 1,147 na askari magereza 343 pamoja na familia zao ambao wote wanategemea
huduma za matibabu kutoka kwenye zahanati iliyopo kwenye gereza hilo hivyo
msaaada huo umekuja kwa wakati.
Naye daktari
wa zahanati iliyopo kwenye gereza hilo, Pantaleo Maumba amesema dawa hizo ni
msaada mkubwa kwani zahanati hiyo inatibu kundi kubwa la mahabusu na wafungwa
ambao wanategemea zahanati hiyo kwa matibabu.
Amesema
msaada huo utatumika kama ulivyokusudiwa na kuitaka mamlaka hiyo kuendelea
kutoa msaada wa vifaa tiba na dawa kwani mahitaji ni makubwa kulingana na kundi
wanalolihudumia.
Mwisho



Comments
Post a Comment