POLISI DODOMA KUKABILIANA NA VITENDO VYA UHALIFU
Muhtasari: Kutokana na kushamiri kwa matukio ya ukatili Mkoani Dodoma dawati la jinsia na watoto la polisi limekuja na kampeni kabambe ya kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto mkoani humo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
DAWATI la jinsia na watoto la polisi mkoa wa Dodoma limekutana kwenye kikao kazi maalum cha kujadili matukio ya ukatili yanayoendelea mkoani humo ili kujua namna ya kukabiliana nayo.
Mkuu wa dawati la jinsia Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni mrakibu msaidizi wa jeshi la polisi Christer Kayombo ameyasema hayo leo alhamisi Septemba 17, 2024 kwenye kikao kazi kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wa kijinsia na watoto Jijini Dodoma.
Christer amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa polisi wa dawati la jinsia na watoto kwa lengo la kuwawezesha kuondoa matukio ya ukatili ambayo yameshamiri katika mkoa wa Dodoma.
“Sisi kama mkoa tuliona ipo haja ya kufanya kitu cha ziada ili kupambana na matendo ya ukatili, tukaamua kuandaa mafunzo haya ili tupate mikakati mipya tutakayo itumia kuondoa hali hii katika mkoa wetu,”amesema Christer.
Amesema mafunzo hayo yatawawezesha kuwafikia wanafunzi na vijana waliopo katika maeneo mbalimbali ili kuwambia juu ya mambo ambayo yana athari kwao na jamii kwa ujumla
Amesema pamoja na mafunzo hayo pia kuna kampeni mbalimbali ambazo zimeanzishwa na dawati hilo ili kupunguza ukatili kwenye jamii ikiwemo kampeni ya nyumba yangu haina mhalifu ambayo inalenga wanafunzi wa shule za msingi mkoani Dodoma.
Amesema kampeni nyingine inaitwa ‘tuwaambie kabla hawajaharibiwa’ yenye lengo la kuwawezesha wanafunzi kufahamu na kuepuka tabia hatarishi kama uzinzi, mimba za utotoni, kulatiwa, kubakwa na matumizi ya bangi hivyo kuwawezesha kumaliza masomo yao salama na kupata ufaulu mzuri.
Amesema kampeni hiyo imelenga kuwafikia wanafunzi wa kidato cha kwanza, kidato cha tano, wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwenye vyuo vikuu na vyuo vya kati ili kuwasaidia kujiepusha na tabia za uhalifu ambazo zitazima ndoto zao.
Christer amesema mafunzo hayo pia yanalenga kulipatia jeshi la polisi mikakati ya kubaini sababu za matendo ya ukatili na namna ya kupambana nayo ili kuyaondoa au kuyapunguza kwa kutumia njia bora ikiwemo kuwakamata wahalifu na kuwaondoa katika jamii kwa kuwapeleka katika maeneo husika ikiwemo mahakamani.
“Jamii haina budi kushirikiana na jeshi la polisi kwa namna mbalimbali ili kuondoa matukio haya ikiwemo kuripoti matukio ya ukatili katika dawati la jinsia na kutoa kila ushirikiano unaohitajika kwa mamlaka husika za kisalama juu ya matendo ya ukatili pindi yanapotokea,” amesema Christer
Kwa upande wake mwakilishi wa Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, ambaye ni mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoa wa Dodoma, Boniface Mbao amesema mafunzo hayo yanafanyika kufuatia ongezeko la matukio ya ukatili katika jamii ikiwemo ubakaji, ulawiti na mauaji hali inayozilazimu mamlaka husika kukaa chini na kutafakari ili kuja na mipango na mikakatai mbalimbali ya kukabilina na matendo haya ili kuyapunguza au kuyaondoa kabisa.
Mbao amesema mafunzo haya yatawashikisha jeshi la polisi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo utakaowasaidia kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii ili kuyaelimisha juu ya ukatili.
“Mafunzo haya yameandaliwa na wadau mbalimbali kama Doyodo, DSW na wizara ya maendeleo ya jamii wanawake jinsia na makundi maalumu kwa lengo la kuwajengea askari uwezo wa kupambana na ukatili katika jamii,”amesema Mbao.
Amesema mafunzo yanalenga kuwajengea polisi uwezo wa Kwenda kushiriki katika kampeni ya tuwaambie kabla hajawajaharibikiwa ambayo yana lengo la kuyafikia makundi mbalimbali ili kuwafundisha tabia njema na maadili mazuri.
“Kampeni hii inalenga kuyafikia makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, shule za sekondari na msingi kwa lengo kuwambia wanafunzi hao kuepuka tabia mbaya na ukiukwaji wa maadili.”amesema.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Vijana Dodoma (Doyodo), Rajabu Nunga amesema taasisi hiyo inaunga mkono juhudi zinazofanywa na jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na watoto katika kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyotokea katika mkoa wa Dodoma.
Amesema mafunzo hayo ni muhimu ili kuwawezesha wakuu wa madawati hayo kujua mbinu na mpya za kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyojitokeza kwenye jamii.
Mwisho…..

Comments
Post a Comment