KUFUNGULIWA KWA MASOKO YA MAZAO NJE YA NCHI FURSA KWA WAKULIMA NCHINI
Muhtasari: Serikali ya Tanzania kuingiza kiasi cha fedha dola za Marekani 3.5 bilioni kwa mwaka kutokana na mauzo ya mazao nje ya nchi.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imesema itaingiza kiasi cha fedha dola za marekani 3.5 bilioni kwa mwaka kwa kuuza mazao ya kimkakati nje ya nchi kwa mwaka.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Septemba 19, 2024 na Naibu waziri wa kilimo David Silinde kwenye hafla ya uzinduzi wa mchakato wa kufungua masoko mapya ya mazao ya kipaumbele Jijini Dodoma.
Silinde amesema hivi sasa nchi imepata kibali cha kuuza mazao tisa ya kiupaumbele kwenye nchi 14 ambayo yataliingizia taifa kiasi cha fedha Dola za Marekani 3.5 bilioni na kuwataka wakulima nchini kuchangamkia fursa hiyo.
Ameyataja mazao hayo ya kipaumbele kuwa ni nanasi, ndizi, tumbaku, parachichi, viazi mviringo, karafuu, pilipili manga, vanilla, na kakao ambayo yatauzwa kwenye nchi 14 duniani.
“Nchi hizo ni pamoja na China ambao wanahitaji vanila na nanasi, India (vanilla na nanasi), Indonesia (karafuu), Singapore (karafuu), Israeli (parachichi), Malaysia (parachichi), Uturuki (nanasi), Brazili (nanasi), USA (kakao), Afrika kusini (ndizi), Zambia (viazi mviringo), Pakstani (tumbaku) na Iraq (tumbaku).”amesema Silinde.
Amesema Serikali kupitia wizara ya kilimo imejipanga kufanya maboresho ili kuondoa vikwazo katika usafirishaji wa mazao ya kilimo yananyohitajika katika mataifa mbalimabali duniani ili kuinua uchumi wa taifa kupitia sekta hii.
Naibu waziri huyo amesema inakadiriwa kuwa uuzaji wa mazao nje ya nchi utaiwezesha serikali kupata jumla ya dola za Marekani 3.5 bilioni ambazo ni sawa Sh10 trilioni za kitanzania ambazo zinaweza kuongezeka kama thamani ya mazao haya itaongezwa.
“Serikali kupitia wizara ya kilimo imejipanga kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuinua sekta ya kilimo na kuimarisha ushindani wa mazao yanayozalishwa nchini katika masoko ya kimataifa kwa kufungua masoko mapya.”amesema.
Amesema changamoto ambayo inatakiwa kutatuliwa ni kuondoa vikwazo vya usafi wa mimea ambavyo vimekuwa changamoto kubwa ya usafirishaji wa mazao ya kilimo katika nchi lengwa na kuikwamisha serikali kupata faida maradufu ya ile ambayo wanaipata sasa.
Aidha waziri Silinde ameweka wazi kuwa zipo fursa za kusafirisha mazao katika nchi mbalimbali lakini bado hawajafanikiwa kutokana na kushindwa kukidhi baadhi ya masharti tangulizi ambayo wanapaswa kuyatimiza kabla ya kuanza kusafirisha mazao hayo.
Mmoja wa wasafirishaji wa mazao nje ya nchi Mohamed Adamjee amesema kufunguliwa kwa masoko ya mazao nje ya nchi yanatoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara kuongeza bidii kwenye shughuli zao za kilimo kwa sababu wana uhakika wa kuuza.
Amesema kitendo cha nchi 14 kufanya biashara ya mazao na Tanzania kinawahakikishia wakulima kufanya biashara kuliko kuwa na nchi chache ambapo yakitokea majanga kama vile vita, magonjwa ya mlipuko au uchumi wa nchi kuyumba kunasababisha biashara kusimama.
“Lakini sasa hivi ukimhamasisha mkulima kulima zao flani unakuwa na uhakika wa soko kwa sababu nchi moja ikitetereka nchi nyingine zinaendelea kununua,” amesema Adamjee
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA) Profesa Joseph Ndunguru amesema ufunguzi wa masoko mapya ya mazao ya kipaumbele katika nchi mbalimbali utapanua wigo wa masoko ya mazao ya kilimo katika masoko ya kimataifa hivyo kuongeza tija kwa wakulima, wazalishaji na wasafirishaji wa mazao ya kilimo Kwenda nje ya nchi.
“Mchakato wa kufungua soko jipya la mazao ya kilimo unaweza kuwa rahisi na wa moja kwa moja kwa baadhi ya mazao au bidhaa zitokanavyo na mazao ya kilimo ambayo hayana viashiria vya visumbufu hatarishi, mchakato huu unaweza kuwa mrefu kwa mazao yenye viashiria vya kuwa na visumbufu hatarishi na vya kikarantini,” amesema.
Amesema hatua mpya za kufungua soko jipya la mazao ya kilimo huanza kwa nchi inayotaka kusafirisha zao husika kwa kuwasilisha ombi katika nchi legwa yakishapokelewa wananchi husika hufanyiwa tathmini za awali na kisha nchi inayoomba kusafirisha zao husika huombwa taarifa zinazoitwa nyaraka za kufungua masoko mapya.
Profesa Ndunguru amesema Mamlaka imefanya majadiliano na makubaliano ya kiitifaki ya afya za mimea zinazohusu makubaliano na nchi nyingine katika kusafirisha mazao husika na kuweka masharti, kanuni na sheria kwenye mazao na bidhaa za kilimo zinazopaswa kusafirishwa Kwenda nchi husika hivi karibuni TPHPA imekamilisha kwa kiwango kikubwa makubaliano na baadhi ya nchi.
Amesema TPHPA itahakikisha kuwa mazao yote yanayozalishwa nchini yanakidhi viwango vya kimataifa pia TPHPA inaendelea kufuatilia na kudhibiti visumbufu vamizi nchini kwa kutumia milipuko inayoweza kutishia kukua kwa mazao ya kilimo ambavyo ni panya, nzige, kweleakwelea na viwavi jeshi.

Comments
Post a Comment