WMA YATOA ELIMU KUHUSU MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI KWA WAKULIMA
Muhtasari: Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) watoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kwenye biashara ya mazao na kuachana na vipimo vya magunia, visado, madebe, makopo na lumbesa ambavyo vinawapa hasara.
Rachel Chibwete, Dodoma
ILI kuwawezesha wakulima kutumia vipimo sahihi wakati wa kuuza mazao yao na kuachana na vipimo visivyo sahihi kama vile magunia, visado, makopo madebe na lumbesa, wakala wa vipimo Tanzania (WMA) umetoa elimu kwa wakulima kuachana na vipimo hivyo.
Akizungumza na wakulima waliofika kujifunza kuhusu vipimo sahihi, Ofisa Vipimo kutoka WMA, Said Ibrahim amesema ni wakati wa wakulima kuachana na vipimo visivyo sahihi na kuanza kutumia vipimo sahihi kwa ajili ya maendeleo yao.
Ofisa Vipimo kutoka WMA, Said Ibrahim akizungumza kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma
Amesema kuna utapeli unaofanywa na baadhi ya watu wa kutumia vipimo visivyo sahihi na hivyo kuwapa hasara wakulima kwani gunia moja linafungwa lumbesa na kuweza kutoa magunia mawili.
Amesema lumbesa huwa inaleta hasara kwa mkulima, kupunguza mapato ya Halmashauri kwa kuwa kilichonunuliwa ni kingi lakini kinacholipiwa ushuru ni kidogo na hivyo kuharibu miundombinu ya barabara ambayo inapitisha magari yenye uzito mkubwa
“Hata kipimo cha magunia siyo sahihi kwa kila bidhaa kwa sababu gunia la kilo 100 la mahindi haliwezi kuwa na uzito sawa na gunia la alzeti kwa hiyo ni vizuri mtumie mizani ambayo imehakikiwa na wakala wa vipimo kupima mazao yenu,” amesema Ibrahimu.
Amesema wakala huo huwa unahakiki mizani yote inayoingia nchini kuanzia bandarini hivyo wakulima wakiona mzani ambao hauna nembo ya WMA watoe taarifa maana utakuwa umechakachuliwa.
Baadhi ya wakulima waliohudhuria kwenye mafunzo hayo wametaka elimu hiyo iende vijijini kwa kuwa ndiyo wazalishaji na wanaumizwa na vipimo visivyo sahihi.
Magreth Ndoje mkazi wa Makutupora jijini Dodoma amesema tangu wanakuwa wanatumia vipimo vya madebe, magunia na visado wakati wa kuuza au kununua nafaka kutoka kwa wakulima bila kujua kuwa wanapunjwa.
Amesema elimu ya kutumia mizani ni nzuri hasa kwa wakulima ambao huwa wanafanyakazi kubwa lakini hawanufaiki nayo wanaonufaika ni watu wengine.
Naye Charles Ngobito mkazi wa Iyumbu jijini Dodoma amesema kuna haja ya kutoa elimu ya matumizi ya vipimo sahihi mashuleni ili kuwajengea uwezo watoto kuanzia umri mdogo wa kujua vipimo sahihi badala ya kutumia vipimo ambavyo siyo sahihi na hivyo kuleta hasara kwa wakulima na watanzania kwa ujumla.
Mwisho

Comments
Post a Comment