TSC YAKABIDHIWA MAGARI KWA AJILI YA KUTEMBELEA WALIMU NA KUJUA CHANGAMOTO ZAO

Muhtasari: Tume ya utumishi wa walimu imetakiwa kutatua changamoto na kero za walimu nchini na kama kuna wenye changamoto za kisaikolojia watafutiwe huduma ya ushauri nasaha ili wawasaidie utekeleza majukumu yao ya kutoa elimu wa Watanzania.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameiagiza tume ya utumishi wa walimu (TSC) kughulikia kero na changamoto za walimu nchini ili kuondoa malalamiko yote ya walimu na kama kuna walimu watakuwa na changamoto za kisaikolojia wawape huduma ya ushauri nasaha.

Mchengerwa ameyasema hayo leo jumapili Agosti 11, 2024  wakati akikabidhi magari 10 kwa makatibu wasaidizi wa wilaya wa tume ya utumishi wa walimu jijini Dodoma na kuwataka kuyatumia magari hayo kuwatembelea walimu kwenye vituo vyao vya kazi ili kujua changamoto walizonazo badala ya kukaa maofisini na kusubiri walimu wawafuate.



Sehemu ya magari 10 ambayo yamewagawiwa kwa makatibu wasaidizi wa Wilaya wa tume ya utumishi wa walimu (TSC) leo Agosti 11, 2024 Jijini Dodoma


Wilaya zilizopata magari ni Rufiji, Nyamagana, Ilala Bukombe, Tanga, Mbeya, Ruangwa, Kilosa na Kaliua kati ya Wilaya 394 zilizopo nchini ambapo serikali imeahidi kupeleka magari kwa wilaya zilizobaki 

Amesema magari hayo ni kitendea kazi cha kuwatembelea walimu kwenye vituo vyao vya kazi na kujua kero, malalamiko na changamoto zao kwani kuna makandokando mengi yanayosababisha walimu wasifanye kazi vizuri.

“Walimu wanapitia changamoto nyingi sana unaweza kusikia mwalimuy amefanya tukio kwa mwanafunzi mpaka ukajiuliza imekuwaje kumbe ana changamoto ya kisaikolojia kwa sababu anafundisha kwenye majengo yaliyochakaa, nendeni mkazungume nao na wale watakaobainika kuwa na tatizo la kisaikolojia wapeni huduma ya ushauri nasaha ili wake sawa,” amesema Mchengerwa.

Amesema anataka walimu wafanye kazi kwenye mazingira mazuri yasiyo na changamoto na watakaoifanya kazi hiyo ni TSC na ndiyo maana serikali imeamua kuwanunulia magari ili waweze kuwafikia walimu kwa urahisi.

Aidha amewataka kujua taarifa zote zinazohusu sekta ya elimu nchini ikiwemo uchakavu wa majengo ya shule, ukatili unaofanyika mashuleni na unyanyasaji unaofanywa kwa walimu na kuchukua hatua badala ya kuzipata taarifa hizo kwenye vyombo vya habari.

Amesema hategemei kupata simu na ujumbe kutoka kwa walimu wakimweleza kuhusu changamoto wanazozipitia wakati ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto zote za walimu kabla hazijamfikia.


“Walimu wana changamoto nyingi, waka kero nyingi wana malalamiko mengi nendeni mkazungumze nao myatatue matatizo yao ili kuwajenga vizuri kisaikolojia hili ni jukumu lenu,” amesema Mchengerwa.

Pia amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwawezesha makatibu wasaidizi wa TSC walioko kwenye maeneo yao kuendesha ofisi zao kwa lengo la kuwahudumia walimu kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi anayeshughulikia elimu, Charles Msonde amesema magari hayo yamenunuliwa kwa fedha za Boost ambapo jumla ya magari yaliyonunuliwa ni 16 ambapo magari matano yamepelekwa Tamisemi na magari 11 yamepelekwa kwenye tume ya utumishi wa walimu kwa ajili ya usimamizi na uboreshaji wa sekta ya elimu nchini.

Naye katibu msaidizi wa TSC kutoka Wilaya ya Nyamagana, Penina Alphonce amesema watatumia magari hayo kuwatembelea walimu na kujua changamoto zao ikiwemo kunyimwa mishahara, likizo na kupandishwa madaraja kwani ndiyo kilio kikubwa cha walimu kwenye madai hayo.

Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI