TEKNOLOJIA YA KISIKI HAI IMEOKOA MITI ZAIDI YA MIL 21 NCHINI
Muhtasari: Kisiki hai chaokoa zaidi ya miti milioni 21 nchini kwenye Mikoa ya Singida, Dodoma, Manyara, na Arusha
Rachel Chibwete, Dodoma
TEKNOLOJIA ya kisiki hai imeokoa zaidi ya miti milioni 21 nchini kwenye Mikoa ambayo haina mvua za kutosha kuotesha miti mipya na hivyo kusaidia kurejesha uoto wa asili kwenye Mikoa hiyo.
Akizungumza kwenye maonyesho ya nanenane Mkoani Dodoma, Ofisa kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Lead Foundation, Hagali Mbulla amesema programu ya kisiki hai imesaidia kurejesha uoto wa asili kwenye Mikoa ya Singida, Dodoma, Manyara na Arusha.
Amesema Mikoa hiyo minne haina mvua za kutosha kuotesha miti mipya na kuimwagilia kwani miti mingi inayopandwa hukauka kwa kukosa maji wakati wa kiangazi.
"Ili kurejesha uoto wa asili tumewaelekeza wakulima kupogolea miti ya asili iliyopo kwenye mashamba yao itakayowezesha miti hiyo kuendelea kukua badala ya kupanda miti mipya ambayo huwa inakauka kwa kukosa maji kwa sababu hii mikoa hupata mvua chache lakini visiki vya miti iliyokatwa ikiwa mikubwa inaweza kuendelea kukua bila shida yoyote," amesema Hagali.
Amesema teknolojia hiyo ni rahisi na imewezesha kuzuia vimbunga vilivyokuwa vinaikumba Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma kila inapofika kiangazi baada ya visiki hivyo kukua na kutengeneza misitu hasa kwenye hifadhi za misitu ya Kijiji na mashamba ya wananchi.
Pia amesema wameleta teknolojia ya kilimo cha makinga maji ambayo husaidia kupunguza mmomonyoko wa ardhi yenye rutuba kuchukuliwa na maji ya mvua pamoja na upepo.
Amesema teknolojia hiyo imesaidia wakulima kupata mavuno ya kutosha kwenye mashamba yao kwani makinga maji hayo yanasaidia kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu na hivyo kusaidia mazao kukua.
Comments
Post a Comment