NIC IMEWATAKA WAKULIMA KUKATA BIMA YA FIDIA ILI KUJILINDA NA MAJANGA YA TABIANCHI
Muhtasari: Shirika la bima la Taifa limewataka wakulima kukatia bima ya fidia mazao yao ili kujikinga na majanga ambayo hayazuiliki.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la bima la Taifa limewataka wakulima wafugaji na wavuvi kukatia bima ya fidia mazao yao ili kujikinga na majanga ambayo hayazuiliki.
Wito huo imetolewa leo Ijumaa Agosti 2, 2024 na Ofisa maendeleo mwandamizi kutoka Shirika la bima la Taifa (NIC), Nicholaus Malakasuka wakati akizungumza kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma.
Ofisa maendeleo mwandamizi kutoka Shirika la bima la Taifa (NIC), Nicholaus Malakasuka akizungumza kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma Leo Agosti 2, 2024
Malakasuka amewataka wakulima, wafugaji na wavuvi kukatia bima ya fidia shughuli wanazofanya ili kujilinda na majanga mbalimbali yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira.
Amesema NIC inatoa bima za fidia kwenye shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuwawezesha wananchi hao kuendelea na shughuli wanazozifanya hata kama watapata hasara kwenye uzalishaji wao.
Amesema mojawapo ya bima ya fidia wanazotoa ni kumfidia mkulima mazao ambayo alikuwa ayapate kwa msimu lakini hakuyapata kutokana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.
"Kwa mfano mkulima amepanga kupata magunia 100 wakati wa mavuno lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake amepata magunia 70 sisi bima tutamfidia mkulima huyo magunia 30 aliyoyakosa kwa kumpa kiasi cha fedha kulingana na bei ya sokoni kwa wakati huo... hii inasaidia mkulima kuendelea na shughuli zake," amesema Malakasuka
Amesema hivyo hivyo kwa wafugaji na wavuvi wanatoa fidia kwa mitumbwi wanayotumia kulia samaki na kwenye vizimba vya kufugia samaki kwa kuwafidia pale wanapopata matokeo tofauti na matarajio yao ili waendelee na shughuli zao za uzalishaji maji.
Amesema NIC inafanyakazi na vyama vya ushirika pamoja na benki zinazotoa mikopo ili kuwapata wenye sifa kwa ajili ya kulipa fidia pale yanapotokea majanga maana wakulima, wafugaji na wakulima ni lazima wafuate taratibu zote za kilimo, ufugaji na uvuvi bora ili wapopata hasara isiwe ni kwa sababu ya uzembe wao.
Mwisho

Comments
Post a Comment