NEMC YAJA NA MRADI WA MAJOSHO KUTUNZA VYANZO VYA MAJI

 Muhtasari: Ili kutunza na kulinda mazingira kwenye vyanzo vya maji, Baraza la Taifa la  Usimamizi wa mazingira (NEMC) limeanzisha miradi ya majosho kwa wafugaji ili kuzuia wanyama kubomoa kingo za mito pale wanapokwenda kunywa maji.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma 


BARAZA la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeanzisha mradi wa majosho kwa wafugaji wanaoishi kwenye vyanzo vya maji na kando ya mito ili kutunza vyanzo hivyo visiharubiwe na wanyama pale  wanapokwenda kunywa maji.


Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mazingira Mkuu kutoka NEMC, Innocent Makomba wakati akizungumza kwenye maonyesho ya wakulima nanenane kuhusu hatua zinazochukuliwa na baraza hilo kulinda vyanzo vya maji nchini Jijini Dodoma.



Ofisa Mazingira mkuu kutoka NEMC Innocent Makomba akizungumza kuhusu uanzishwaji wa majosho kwenye maeneo ya wafugaji ili kulinda vyanzo vya maji nchini kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma leo Agosti 6, 2024


Makomba amesema kunywesha maji kwenye vyanzo vya maji na kwenye mito kunasababisha wanyama kuharibu kingo na kusababisha uharibifu wa mazingira kwa hiyo ili kulinda vyanzo hivyo baraza limeanzisha majosho ya kunywesha wanyama ili wasifike kwenye vyanzo vya maji.


"Kingo za mito huwa zinaharibika kutokana na wanyama wanapokwenda kunywa maji kwa sababu huwa kwenye makundi makubwa, kwa kuliona hilo NEMC tumeanzisha mradi wa kuweka majosho kwenye maeneo ya wafugaji ili badala ya wanyama kushuka mtoni kunywa maji wayakute yameshajazwa kwenye majosho  hii itasaidia kutunza kingo za mito na vyanzo vya maji," amesema Makomba.



Ofisa Mawasilino kutoka NEMC, Martha Kawishe akigawa vipeperushi kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mazengo iliyopo Jijini Dodoma walipotembelea Banda hilo ili kujifunza habari za mazingira kwenye maonyesho ya wakulima nanenane 


Amesema vyanzo vya maji na mito inategemewa na kundi kubwa la wananchi na siyo wafugaji pekee yao hivyo ni lazima vilindwe na kutunzwa kwa hali na mali  visichafuliwe au kukauka kwa ajili ya matumizi endelevu.


Amesema mradi huo ni sehemu ya mpango mkakati wa kutunza vyanzo vya maji visichafuliwe kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na ufugaji wa wanyama.


Pia ameshauri wakulima kuachana na kilimo cha kuhama hama kwani huwa kinahusisha ukataji wa miti kwenye eneo kubwa kwa ajili ya kufungua mashamba mapya na badala yake wafuate kanuni za kilimo bora ili waboreshe ardhi na kupata mavuno mengi.


Kwa upande wake Ofisa Mazingira kutoka NEMC Mariam Shayo amesema uchafuzi wa mazingira ni pamoja na kutupa chupa za plastiki baharini ambazo zinahatarisha uhai wa viumbe hai vinavyoishi baharini kwa kuwa chupa hizo huwa haziozi kwa haraka kama ilivyo kwa bidhaa za karatasi.


Pia amewataka wananchi kuepukana na matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku na serikali ili kutunza mazingira kwani mifuko hiyo ina madhara kama italiwa na mifugo kwani inaweza kusababisha vifo.


Naye Juhudi Ezron amesema baraza hilo lina wajibu wa kusimamia mazingira pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira ili waweze kujikinga kwa kupanda miti kwa wingi kwani ndiyo chanzo cha utunzaji wa mazingira na kujiepusha na majanga kama vile vimbunga na mabadiliko ya tabia nchi.


Mwisho.....

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI