MAJALIWA ATOA MAAGIZO MANNE KWA WIZARA YA KILIMO NA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI ILI KUKUZA SEKTA HIYO

 

Muhtasari: Maonyesho ya kilimo, ufugaji na uvuvi nanenane yamezinduliwa leo Jijini Dodoma katika viwanja vya Nzuguni ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo manne kwa wizara za kilimo, mifugo na uvuvi, benki ya kilimo (TADB) na maofisa ugani kuwafikia wakulima na kuwasaidia kutafuta masoko ya bidhaa zao.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua maonyesho ya kilimo, mifugo na uvuvi maarufu nanenane na kuziagiza Wizara za kilimo, mifugo na uvuvi kuendelea kusimamia uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambayo yatawawezesha kufanya shughuli za kilimo, mifugo pamoja na uvuvi katika eneo la uwanja huo kwa kipindi kirefu.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo alhamisi Agosti 1, 2024 wakati akifungua maonyesho ya kilimo, mifugo na uvuvi kwenye uwanja wa nanenane yanayofanyika kitaifa Nzuguni Jijini Dodoma.

Amesema wakiharibu mazingira kwenye maeneo hayo hawatalima kwa sababu hawatapata maji ya umwagiliaji, mito na maziwa itakauka na kuagiza suala la utunzaji wa mazingira liwe ni ajenda ya kudumu kwenye wizara hizo na iende kwenye makundi yote ya kilimo, mifugo na uvuvi na vyama vya ushirika.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua shamba la alzeti lililopo kwenye uwanja wa maonyesho ya kilimo nanenane Jijini Dodoma leo Agost 1, 2024


Amezitaka Wizara hizo pia kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili wafugaji wabadilishe muundo wao wa ufugaji na wavuvi wavue kwa teknolojia mpya lakini wapate mazao mengi.

“Natambua zuio mliloliweka ziwa Tanganyika kwa kutovua kwa nyakati ambapo tunaona linakwenda kuishiashia nadhani mwisho mwezi huu mlizuia kwa miezi mitatu ili wananchi wasivue kwa wakati huo kwa lengo la kutaka samaki wazaliane ili watakapoanza kuvua wapate samaki wengi wenye ukubwa utakaoweza kutupatia fedha,” amesema Waziri Mkuu.

Pia ameiagiza benki ya maendeleo ya kilimo (TADB )iweke mkakati mahususi ya kuwafikia wananchi wajue benki hiyo iko wapi na pale ambako hakuna benki wakulima watawapataje kwa sababu wakulima hao wanahitaji huduma kule walipo wasigharamie kulipa nauli kwenda umbali mrefu kutafuta benki.

“Hebu jipangeni wafikieni wakulima, wafugaji na wavuvi na kwenye banda lenu hapa fanyeni kazi ya kuwaelimisha na kuwahabarisha wapi mlipo na mikopo inapatikanaje tunatamani kuona watanzania wengi wakiingia kwenye kilimo ambacho leo kimethibitisha kwamba ndiyo mkombozi wa maisha yetu na uchumi wetu,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amewaagiza maofisa ugani popote walipo watumie mifumo ya kidigitali kuwafikia wakulima wawaambie namna nzuri ya kulima na kufuga na kuvua, namna nzuri ya kutunza mazao yao lakini pia namna ya kupata masoko kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao.

Amesema kwa kuwa maofisa ugani hao wako kwenye Halmashauri zote wawasaidie wakulima namna ya kupata mitaji kwenye taasisi za kifedha ili waweze kuzungumza lugha moja kwa kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi.



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kulia) akipata maelezo kutoka kwa waziri wa kilimo Husssein Bashe alipokwenda kufungua maonyesho ya wakulima nanenane kwenye viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma 


Kwa upande wake waziri wa kilimo Hussein Bashe amesema viwanja vya maonyesho ya wakulima vimefanyiwa ukarabati mkubwa ili kuwawezesha wakulima nchini kwenda kujifunza kilimo bora kwa mwaka mzima.

Amesema kwa sasa sekta ya kilimo imekuwa kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 4.2 mwaka huu wa fedha huku lengo likiwa ni kufikisha asilimia 5 na ikifika mwaka 2030 sekta hiyo ikue kwa asilimia 10.

Amesema kwa sasa sekta ya kilimo ina uhakika wa soko na kwa mwaka huu serikali imefanikiwa kuuza tani 600,000 za mahindi nchini Zambia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendegu amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi mkoa huo umeendelea kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira ambapo kwa kupitia miradi mkubwa ya umwagiliaji  yenye thamani ya Sh54 bilioni imeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 17 hadi hekta 21,400 sawa na asilimia 43 ya eneo lote linalofaa kwa umwagiliaji.

Mwisho.

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI