IDADI YA MIFUGO NCHINI IMEONGEZEKA NA KUFIKIA MIL181.9

 Muhtasari: Serikali imetaja ongezeko la idadi ya wanyama wa kufugwa nchini ambayo kwa mwaka 2023/24 imeongezeka na kufikia milioni 181.9 kutoka mifugo 173.1 mwaka 2022/23.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amesema idadi ya mifugo nchini imeongezeka kutokana na usimamizi mzuri unaofanywa na sekta ya mifugo na uzalishaji wa mazao ya mifugo kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Mnyeti ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 2, 2024 kwenye maonyesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Amesema hadi kufikia mwaka 2023/2024 Tanzania ilikuwa na jumla ya ng’ombe milioni 37.9, mbuzi milioni 27.6, kondoo milioni 9.4, nguruwe milioni 3.9 na kuku milioni 103.1 ambapo kuku wa asili ni milioni 47.4 na kuku wa kisasa milioni 55.7. 



Naibu waziri wa mifugo na uvuvi Alexander Mnyeti akizungumza kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma 

Naibu waziri huyo amesema ongezeko hilo ni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2022/23 ambapo kulikuwa na ng’ombe 36.6, mbuzi milioni 26.6, kondoo milioni 9.1, nguruwe milioni 2.9. na kuku milioni 97.9.

Pia mesema sekta ya uvuvi inaendelea kuwa muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji 34,057 na takriban watanzania Milioni sita wanajihusisha na shughuli mbalimbali zinazohusiana na uvuvi katika mnyororo wa thamani.

“Katika mwaka 2023/2024 serikali ilitoa jumla ya Sh60 bilioni kutekeleza mradi wa kuwapatia wavuvi mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya ununuzi wa boti za kisasa za uvuvi na zana zake, ufugaji samaki kwenye vizimba na uzalishaji wa zao la mwani ambao unasimamiwa na benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB),” amesema Mnyeti

Aidha amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea kutekeleza programu ya utoaji wa mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa vijana nchini ambayo inatarajiwa kuwezesha vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.

“Katika mwaka 2022/2023 jumla ya vijana 200 wamepatiwa mafunzo hayo na mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana 750, nitoe wito kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo itakayowawezesha kiuchumi,” amesema. 

Amesema katika maonyesho hayo kutakuwa na mashindano ya mifugo ambayo yana lengo la kuwahakikishia wafugaji kuwa matumizi ya teknolojia ya ufugaji yanawezekana katika mazingira ya kufuga kwenye maeneo anayoishi na  kushawishi matumizi ya teknolojia ya ufugaji bora.

Mnyeti amesema maonesho hayo  huwezesha wafugaji kujenga imani kwa wataalamu wa ugani kwa kuwahakikishia kuwa ushauri wao ni wa thamani na wenye tija pia, husaidia kujenga imani kwa wafugaji kuhusiana na matumizi sahihi ya teknolojia za ufugaji bora zinazotolewa na watafiti hapa nchini na kuwafundisha kutumia mbinu hizo kuboresha ufugaji wao. 

Kwa upande wake mkurugenzi wa benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) Japhet Justine amesema hadi kufikia Aprili mwaka 2024, benki ya TADB imetoa mkopo wa Sh 15.82 bilioni ambapo mikopo hiyo ilielekezwa kwenye maeneo ya ufugaji wa ngómbe, kuku na nguruwe; uzalishaji wa malisho na vyakula vya mifugo; unenepeshaji wa mifugo na uchakataji wa mazao ya mifugo.

Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI