BOT KUJA NA KAMPENI KABAMBE YA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUJIEPUSHA NA MIKOPO UMIZA

Muhtasari: Benki kuu ya Tanzania (BOT) yaja na mbinu ya kuwaelimisha wakulima jinsi ya kuondokana na mikopo umiza ambayo haina faida kwenye shughuli zao za uzalishaji mali.

Rachel Chibwete, Dodoma

ILI kuwaepusha wakulima na mikopo umiza benki kuu ya Tanzania (BOT) imekuja na kampeni ya kutoa elimu ya kujiepusha na mikopo hiyo ambayo huwa inawarudisha nyuma wakulima badala ya kuwaletea maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Agosti 2, 2024 na Ofisa wa idara ya usimamizi wa huduma ndogo za fedha (BOT), Deogratius Mnyamani, wakati akizungumza na Mwananchi Digital kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma.



Ofisa wa idara ya usimamizi wa huduma ndogo za fedha (BOT), Deogratius Mnyamani akizungumza kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma 

Mnyamani amesema wakulima ni waathirika wa mikopo umiza inayotolewa na watu ambao hawana leseni za kutoa huduma za kifedha na hivyo kujikuta fedha zao zote zinachukuliwa na hao watu.

“Kuna watu wanatoa mikopo na kutoza riba hadi asilimia 50 kwa mwezi hii haiwezekani kwa sababu hakuna biashara itakayokuingizia kipato kikubwa namna hiyo kwa mwezi nab ado bishara yako iendelee kusimama na ndiyo maaa tupo hapa kutoa elimu ya mikopo salama kwa wakulima,” amesema Mnyamani na kuongeza kuwa,

“Tunajua kuwa ili kilimo, mifugo na uvuvi viende mbele inahitajika mikopo lakini tunawashauri wakakope kwenye taasisi zilizosajiliwa na benki kuu badala ya kukopa kwa watu ambao hawajasajiliwa na mwisho wake wanafilisika.”

Amesema hivi karibuni BOT itakuja na kampeni maalum ya kuwaelisha watu kujiepusha na mikopo umiza itakayojulikana kama ‘zinduka, usiumizwe kopa kwa maendeleo’ kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kukopa kwa malengo.

Amesema wapo baadhi ya watu wanakopa kwa ajili ya kufanya sherehe, au kumtuza rafiki yake mwisho wa siku anashindwa kurejesha mkopo kwa sababu hakufanyia kitu cha maana.

Amesema zipo taasisi nyingi za kutoa mikopo zilizosajiliwa na BOT hivyo kama mtu anahitaji mkopo aende akajiridhishe kama kweli taasisi hiyo imesajiliwa na inatoza riba kama ilivyoelekezwa ya asilimia 3.5 kwa mwezi.

Amesema faida za kukopa kwenye taasisi zenye leseni wanaweza kuwashtaki pindi watakapokwenda kinyume na leseni zao za uendeshaji ambapo adhabu yake inaweza kuwa kufungiwa kutoa huduma.

Aidha amewashauri watanzania ambao wanakopa kwenye taasisi za mikopo kubaki na mkataba wa makubaliano ili kama kutatokea changamoto yoyote aweze kusaidiwa kupitia mkataba alioingia.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya mawasiliano wa BOT, Vicky Msina amesema baadhi ya wakulima huwa wanatapeliwa na taasisi zinazotoa mikopo mitandaoni kwa kuwataka waweke kiasi flani cha fedha kisha watapata nyingi na matokeo yake huwa wanatapeliwa.

Amesema wakulima, wafugaji na wavuvi ni kundi la watu ambao wana fedha nyingi lakini hujikuta maskini kwa kuingia kwenye mikono ya matapeli ambao huwa wanawakopesha kwa riba kubwa hivyo badala ya kufanikiwa wanaendelea kurudi nyuma.

Mwisho……

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI