BILA TASAF NISINGEFIKA CHUO KIKUU KUSOMEA UHANDISI AMBAYO NI NDOTO YANGU
Muhtasari: Mwanafunzi wa uhandisi wa Mawasiliano kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Habiba Maramoja ameelezea namna Mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) ulivyomsaidia kutimiza ndoto zake kwani bila wao asingeweza kusoma chuo kikuu.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayesomea uhandisi wa mawasilino, Habiba Maramoja amesema kama familia yao isingeingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) asingeweza kufikia ndoto zake za kusomea kozi hiyo kutokana na umaskini waliokuwa nao kabla ya kuingizwa kwenye mpango.
Akizungumza leo Alhamis, Agosti 8, 2024 kwenye maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma, Habiba amesema familia yao ni miongoni mwa kaya maskini zilizosaidiwa na Tasaf kwani walikuwa hawawezi kupata milo mitatu kwa siku kwa kuwa walikuwa wanaishia mlo mmoja kwa siku na wakati mwingine walikuwa hawapati kabisa.
Amesema kaya yao iliingia kwenye mpango wa Tasaf mwaka 2014 na wakati huo alikuwa kidato cha kwanza hivyo fedha walizokuwa wanapewa ziliwasaidia kumudu baadhi ya mahitaji ya shule ambayo hapo awali wazazi walikuwa hawana uwezo wa kununulia na kusababisha kaka yake mkubwa kuishia darasa la saba, mwingine kuishia kidato cha nne na mmoja kukatisha masomo akiwa kidato cha pili kutokana na ugumu wa maisha.
Amesema fedha hizo zilimsaidia yeye kusoma elimu ya sekondari kwa utulivu kwani alikuwa akipatiwa mahitaji ya shule kutoka kwenye fedha zinazotolewa na Tasaf.
Habiba Maramoja ambaye ni mtoto wa mnufaika wa mpango wa kunusurubkaya maskini nchini (Tasaf) (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jinsi mfuko huo ulivyomwezesha kufika chuo kikuu. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrack Mziray
“Wazazi wangu ni wazee hasa baba yangu ni mtu mzima sana, hawezi kufanya kazi na mara yangu ya mwisho kumwona akifanya kazi ni nilipokuwa darasa la nne…. kwa sasa hana nguvu za kufanya kazi aliyebaki ni mama ambaye siyo mzee sana ila hali ya maisha ndiyo siyo nzuri,”
“Kwa hiyo tulipoingia kwenye mpango wa Tasaf mama ndiye aliyekuwa anachukua fedha zilipokuwa zinatoka, kila baada ya miezi miwili alikuwa anapokea Sh72,000 kwa sababu alikuwa na watoto watatu ambao wapo shuleni, mimi kaka yangu na mdogo wangu kwa kweli tangu wakati huo tulianza kuona mwanga wa maisha,” amesema Habiba.
Amesema kutokana na fedha walizokuwa wanazipata mama yao alianzisha biashara ya kuuza vitafunwa alivyokuwa anauza kwenye shule za msingi zilizopo Mbagala ambapo alikuwa anapata faida iliyokuwa inatunza familia.
Amesema baada ya kumaliza elimu ya sekondari alifaulu kwenda kidato cha tano ambapo kupangiwa kwenda shule ya Nyantakala iliyopo Mkoani Kagera kwa mchepuo wa masomo ya sayansi ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM).
Amesema kutokana na fedha ya Tasaf aliweza kusoma bila shida yoyote kwani familia ilikuwa na uwezo wa kumgharamikia mahitaji yake yote kupitia fedha ya ruzuku pamoja na biashara waliyokuwa wanaifanya.
Amesema alimaliza masomo yake kwa kupata ufaulu wa daraja A na alichaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye kozi ya uhandishi wa Mawasiliano kwa miaka minne.
Habiba ambaye ndoto yake kubwa ilikuwa na kuwa mhandisi wa masula ya mawasiliano tangu utoto amesema familia yake isingekuwa kwenye mpango wa Tasaf asingeweza kusoma chuo kikuu hata kama angepata mkopo wa asilimia 70.
“Bahati nzuri wakati tunajiunga na chuo kwa wale ambao tunatoka familia zenye hali duni tuliambiwa tuambatanishe na ile fomu ya Tasaf kwa hiyo wakati wa maombi niliambatanisha na hiyo fomu ambapo nilifanikiwa kupata mkopo kwa asilimia 100,” amesema Habiba.
Amesema kozi anayosoma ada yake ni Sh1.5 kwa mwaka hivyo kwa hali ilivyo nyumbani kwao asingeweza kugharamia hiyo ada lakini kwa sababu familia ipo kwenye mpango amepata mkopo na hivi karibuni atatimiza ndoto yake ya muda mrefu.
Amesema fedha za kujikimu ambazo anapata huwa zinamsaidia kupata mahitaji yake madogo madogo na nyingine amemtumia mama yake na kumwongezea mtaji wa kukopesha vitenge na hivyo familia yao kwa sasa inaimarika kiuchumi siyo kama ilivyokuwa miaka kumi nyuma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrack Mziray amesema mpango huo una ubia na bodi ya mikopo nchini (HESLB) ambapo wanafunzi wanaotoka kwenye familia zilizopo kwenye mpango wa Tasaf huwa wanapata asilimia 100 ya mkopo ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu.
Amesema mojawapo ya wanafunzi hao ni pamoja na Habiba ambaye anatoka kwenye familia ambayo inapata ruzuku kutoka Tasaf na kwa kupitia ubia huo ameweza kupata mkopo unaomwezesha kusoma masomo yake ya elimu ya juu ambapo kama hangekuwa kwenye mpango asingeweza kupata mkopo huo.
Mziray amesema mpango huo unahudumia takribani kaya maskini milioni 1.3 tangu kuanzishwa kwake na mpaka sasa zaidi ya walengwa 400,000 wameondolewa kwenye mpango baada ya kufanyiwa tathmini na kuonekana hali zao za maisha zimeboreka.
Amesema pia wameunda vikundi vya wanufaika wa Tasaf ambavyo vimewawezesha kufanya biashara ndogo ndogo na kwa kutumia wataalam wa biashara na uchumi huwawezesha kujua mahitaji ya bidhaa zinazohitajika sokoni na wao kutumia fursa hiyo kuuza.
Mwisho.

Comments
Post a Comment