ASA YAJA NA MBEGU YA NGANO INAYOSTAWI MKOA WA DODOMA
Muhtasari: Wadau wa sekta ya kilimo wamekuja na teknolojia mbalimbali za kilimo za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuwawezesha wakulima kulima kisasa na kupata mazao bora.
Rachel Chibwete, Dodoma
WADAU wa kilimo wamekuja na teknolojia mbalimbali za kilimo ambazo zitawasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kujiepusha na uharibifu wa mazingira.
Hayo yamebainika leo jumapili Agosti 4, 2024 kwenye maonyesho ya kilimo nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye maonyesho hayo, Ofisa kilimo kutoka wakala wa mbegu nchini (ASA), Benjamin Mfupe amesema wamekuja na mbegu za ngano ambazo zimeonyesha mafanikio makubwa kwenye ardhi ya Dodoma ambayo haina historia ya kulima zao hilo.
Ofisa kilimo kutoka wakala wa mbegu nchini (ASA) Benjamin Mfupe akionyesha zao la alzeti kwenye kitalu kilichopo kwenye viwanja vya maonyesho ya wakulima nanenane Jijini Dodoma
Amesema wamepanda ngano kwa majaribio kwenye vitalu vilivyoko kwenye maonyesho hayo ili kuona kama utamea vizuri na matokeo yamekuwa mazuri kuliko matarajio yao.
"Tumekuja na aina tatu za mbegu za ngano ambazo ni mbegu ya sifa na juhudi zinazozalishwa Tanzania na mbegu ya SST884 ambayo imetoka Zambia na matokeo yake yamekuwa mazuri kuonyesha kuwa hata Mkoa wa Dodoma unaweza kulima zao la ngano," amesema Mfupe.
Amesema mbegu zote zimepandwa kwa siku moja lakini zimekomaa kwa wakati tofauti hivyo wakulima wataelekezwa kuhusu mbegu hizo pamoja na kiasi cha mavuno yatakayopatikana ili achague mwenyewe aina ya mbegu atakayopendezewa naye.
Amesema pia wamekuja na mbegu ya mtama aina ya Tarisor 2 ambayo haishambuliwi sana na ndege kama ilivyo kwa mtama aina ya mecia ambayo hushambuliwa na ndege.
Amesema baada ya malalamiko ya muda mrefu ya wakulima kuhusu mtama wa aina ya mecia kuliwa na ndege na kuwapatia mavuno kidogo walilazimika kufanya utafiti na kuja na mbegu hiyo ambayo haishambuliwi na ndege.
Ametaja sifa ya mbegu hiyo kuwa haina weupe kama ilivyo kwa mecia hivyo haiwavutii ndege kuishambulia na hivyo kuleta mazao mengi kwa mkulima.
Amesema pia wamekuja na mbegu fupi ya alzeti ambayo inazaa kuliko ile ndefu na inazalisha mafuta mengi kwa bei ndogo ya ruzuku kutoka serikalini.
Mbali na hilo amesema wakala huo una mbegu ya kitunguu aina ya Mang'ola red au Bombay red ambacho ni imara kuliko m egu nyingine kwani kina maganda matatu hivyo hakiharibiki haraka

Comments
Post a Comment