PBZ YATOA MSAADA WA JOKOFU LA KUHIFADHIA DAMU
Muhtasari: Msaada huo utawezesha kuanzishwa kwa huduma ya mama na mtoto pamoja na upasuaji kwa akina mama wanaojifungua katika kituo hicho cha afya ambacho hakijaanza kutoa huduma ya kujifungua kutokana na kutokuwa na jokofu la kuhifadhia damu
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
KITUO cha afya kilicho chini ya jeshi la polisi mkoa wa Dodoma kitaanza kutoa huduma ya mama na mtoto kuanzia Agost 1, mwaka huu baada ya kukamilisha mahitaji yote yanayotakiwa katika wodi hiyo ikiwemo jokofu la kuhifadhia damu kwa wenye uhitaji.
Kauli hiyo imetolewa leo jumatatu Julai 1, 2024 na mganga mfawidhi wa kituo hicho Dk Jackson Shoo wakati akipokea msaada wa jokofu la kuhifadhia damu lenye uwezo wa kuhifadhi lita 360 kwa wakati mmoja kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Jijini Dodoma.
Dk Shoo amesema kituo hicho cha afya kina wodi ya kujifungulia akina mama lakini bado halijaanza kufanya kazi kutokana na kutokamisha baadhi ya mahitaji muhimu ikiwemo jokofu la kuhifadhia dawa.
"Tulikuwa tunapata changamoto tukipata mama mjamzito hapa kwani tulikuwa tunalazimika kumpa rufaa aende hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa sababu tulikuwa hatuna damu endapo mama angehitajika kuongezewa damu wakati wa kujifungua lakini sasa tutatoa huduma Bora kwani mahitaji yote muhimu yameshapatikana hapa," amesema Dk Shoo na kuongeza kuwa,
"Damu itakayohifadhiwa hapa haitasaidia wagonjwa wanaotibiwa hapa tu Bali utasaidia hata wale ambao wapo kwenye maeneo mengine hivyo uwepo wa jokofu hili ni mkombozi kwa wananchi wa Dodoma."
Amesema kutokana na kuanza kutoa huduma ya mama na mtoto kwenye kituo hicho, wataanzisha kituo cha kuchangisha damu wakianza na watumishi wa hospitali hiyo na watu wengine kutoka nje ili kuhakikisha benki ya damu kwenye kituo hicho haikauki.
Kwa upande wake Meneja wa tawi wa PBZ, Mwanaharusi Shein amesema msaada huo umekuja baada ya kituo hicho cha afya kuomba msaada wa jokofu hilo la kuhifadhia damu ili waweze kufungua wodi ya mama na mtoto.
Amesema benki hiyo ina wajibu wa kuihudumia jamii inayowazunguka hivyo msaada huo ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii kwani wananchi wengi hasa akina mama na watoto watapata huduma kupitia msaada huo.
Amesema jokofu hilo limegharimu kiasi cha Sh7 milioni.
Naye Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya ameishukuru benki hiyo kwa msaada na kuitaka kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika huduma mbalimbali inayozitoa kwa jamii.
Mwisho......

Comments
Post a Comment