MWONGOZO WA KUVUA SAMAKI KWENYE MAJI MADOGO WATOLEWA
Muhtasari: Wizara ya mifugo na uvuvi kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa, ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji na Ofisi ya makamu wa Rais Mazingira zimetakiwa kutoa elimu kuhusu uvuvi endelevu kwenye maji madogo na maeneo oevu ili kulinda na kutunza rasilimali hiyo ambayo imeajiri watu wengi nchini.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
WADAU wa uvuvi nchini wametakiwa kutoa elimu ya uvuvi endelevu kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini ili kufanya uvuvi huo uwe endelevu na wao waendelee kujipatia kipato bila kuvunja sheria na miongozo iliyopo.
Kauli hiyo imetolewa leo ijumaa jUNI 28, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Edwin Mhede wakati akizungumza na wadau wa uvuvi kwenye kikao cha kupitia rasimu ya mwongozo wa usimamizi wa uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu Jijini Dodoma.
Dk Mhede amesema wavuvi wengi hawajui sheria na miongozo kuhusu uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu inavyotumika hivyo ni wajibu wa Wizara ya mifugo na uvuvi kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa, ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya makamu wa Rais Mazingira kutoa elimu ili uvuvi huo uwe endelevu na wenye manufaa kwa Taifa.
“Wavuvi wengi wanafanya shughuli zao bila kujua miongozo na sheria inayotumika kufanya kazi kwenye maeneo hayo, wanachojua wao ni kupata kipato kupitia shughuli za uvuvi hivyo ni jukumu letu kutoa elimu kuhusu miongozo na sheria zinazotumika kwenye uvuvi huo ili wavuvi wafanya kazi kwa tija na si kuharibu maeneo hayo,” amesema Dk Mhede
Amesema kutokana na kutokuwa na elimu wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye maji madogo wamekuwa wakitumia zana za uvuvi zilizokatazwa kufanya uvuvi haramu kama vile kutumia kokoro, mgono nyavu ndogo na nyingine ambazo siyo salama kwa shughuli za uvuvi endelevu.
Amesema mwongozo, kanuni na sheria zilizotungwa hazihusiani na uvuvi kwenye maji mengi kama vile ziwa Victoria, Ziwa nyasa, Ziwa Tanganyika, Bwawa la Mtera, Bwawa la Nyerere na Bwawa la nyumba ya Mungu.
Amesema japo kuna usimamizi mdogo wa sheria na miongozo kwenye uvuvi wa maji madogo haizuii sheria hizo kufuatwa na wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye maeneo hayo na kuachana na zana za uvuvi haramu ili kulinda rasilimali zilizoko kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi msaidizi kitengo cha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, Bugomba Kimasa amesema shughuli za uvuvi kwenye maji madogo zinawapatia wananchi chakula na kipato hivyo ni lazima kuwe na mwongozo ili shughuli hiyo iwe endelevu.
Amesema maji madogo ni yale ambayo kuna kipindi huwa yanakauka hasa kipindi cha kiangazi na kipindi cha mvua huwa yanajaa.
Amesema lengo la kuweka mwongozo huo ni kuzitambua shughuli za uvuvi zinazofanywa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kujipatia chakula na kipato kwa watu wanaojishughulisha na uvuvi.
Naye aziza Mumba kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma, amesema mkoa huo una maeneo mengi ya uvuvi wa maji madogo likiwemo Bwawa la Bahi ambalo huwa linafungwa kutokana na maji kukauka na hivyo nyavu za kuvulia samaki zinazotakiwa kushindwa kuvua samaki na hivyo wavuvi kuamua kutumia nyavu zilizokatazwa na serikali ili waendelee kuvua bila kujua athari zake.
Mwisho


Comments
Post a Comment