KUTOKA KUOMBA OMBA HADI KUMILIKI DUKA LAKE
Muhtasari: Mwanamke huyo ambaye ni mlemavu wa viungo kwa sasa anamiliki duka ambalo limemsaidia kuachana na kuomba msaada kwa watu na sasa anaihudumia familia yake ya watu wanne kutokana na biashara hiyo ya duka.
Na Mwandishi Wetu, Chamwino.
MKAZI wa Kijiji cha Majeleko
kilichopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, Melea Obed ambaye ni mlemavu wa
viungo amejikuta akiachana na kazi ya kuomba misaada kwa watu baada ya kupata
ufadhili wa kufunguliwa duka la kuuza mahitaji ya nyumbani.
Akizungumza na Kirimbo Blog leo
jumatano, Julai 2024 Melea ambaye hawezi kukaa wala kutembea kutokana na
ulemavu alionao amesema kabla ya kufunguliwa biashara ya duka alikuwa anashinda
ndani hata miezi minne bila kutoka nje.
Amesema hiyo inatokana na kutokuwa
na uwezo wa kufanya shughuli yoyote kwa kuwa hawezi kushika kitu wala kutembea
kwa miguu yake hivyo alikuwa anategemea wamtoe nje na kumrudisha ndani na
alipokosa wa kumtoa nje alikuwa anakaa ndani bila kutoka nje hata miezi minne
mfululizo.
“Nimekuwa hivyo kwa miaka 14, mimi
nilikuwa ni wa kushinda ndani tuu hata mikutano ya kijiji nilikuwa siwezi
kwenda nasubiri waliokwenda huko warudi waje wanihadithie yaliyozungumzwa huko,
maana nilikuwa nasikia tu matangazo ya mikutano lakini uwezo wa kwenda huko
nilikuwa sina,” amesema Melea.
Mwanamke huyo mwenye watoto wawili
amesema hali ya maisha ilikuwa mbaya kwani watoto wake walikuwa wakiishiwa
kalamu au madaftari walikuwa wakiomba kwa wasamaria wema ili wawasaidie kwa
kuwa hakuwa na uwezo wa kuwahudumia.
“Hata maisha yangu yote yalikuwa
ni ya kuomba kwa sababu siwezi kufanya kazi yoyote hali iliyosababisha mwanangu
mkubwa kubeba ujauzito wakati anatutafutia chakula na hata aliyempa ujauzito
huo hajulikani,” amesema Melea.
Melea amesema maisha yake yalianza
kubadilika baada ya watu wa shirika lisilo la kiserikali la Brac Maendeleo
Tanzania kufika kijijini hapo kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu na
wanaoishi kwenye umaskini uliokithiri.
Amesema wakati wakiwatafuta watu
wa aina hiyo ili wawasaidie ndipo na yeye alipokutanishwa nao na kutokana na
hali aliyokuwa nayo walimtengenezea kiti mwendo ili aweze kukitumia kutembea
kwenye maeneo mbalimbali badala ya kushinda ndani amelala.
Amesema baada ya kupewa mafunzo ya
kuwezeshwa kiuchumi alichagua mradi wa kuuza duka na kufuga bata ambao
umebadilisha maisha yake kwani hivi sasa anahudumia familia yake kwa kile
anachokipata kwenye biashara zake na ameachana na kuombaomba ili aishi.
Amesema anasaidiana na binti yake
kwenye biashara hiyo huku kiti mwendo alichopewa kikimsaidia kuzunguka maeneo
mbalimbali kwa ajili ya kutafuta bidhaa za kuweka dukani kwake badala ya kukaa
na kusubiri kuletewa mzigo bila kujua thamani yake.
Amesema biashara hiyo imemsaidia
kuishi yeye na mabinti zake wawili ambapo mmoja ni mwanafunzi wa shule ya
sekondari pamoja na mjukuu wake mmoja.
Mbali na hilo amesema pia
amejiunga kwenye vikoba ambapo wenzake walimchagua kuwa mwenyekiti wao mahali
ambapo wanaweza kukopa na kuongeza mitaji kwenye biashara zao.
Melea amesema kwa sasa anahitaji
jengo analolitumia kama duka lenye
ulinzi zaidi kwani alilonalo kwa sasa analazimika kuingiza bidhaa ndani baada
ya muda wa kuuza kuisha na yeye hana nguvu za kubeba kutokana na ulemavu
alionao na hata watoto wake bado wadogo hawawezi kubeba mizigo mizito kama
mifuko ya sukari na unga.
“Natamani ningepata jengo imara
ambalo nitakuwa nafungia bidhaa ndani kwa sababu hili la sasa haliko imara kwa
sababu limejengwa kwa mbao hivyo inakuwa rahisi mtu kuvunja na kuiba….lakini
pia ningepata umeme wa uhakika ambao utanisaidia kuuza mpaka usiku kwa sababu
kwa sasa natumia tochi ambayo haina mwanga wa kutosha,” amesema Melea.
Mtendaji wa kijiji cha Majeleko
Lidya Makasi amesema ni kweli wanatambua changamoto anazokutana nazo Melea
katika kuboresha biashara zake lakini wanashindwa kuboresha mazingira kwa
sababu nyumba anayoishi siyo ya kwake bali kuna msamaria mwema amempa aishi
hapo.
“Hatuwezi kufanya maboresho
ikiwemo kuvuta umeme au kujenga jengo la kudumu kwenye nyumba ya mtu bila
ridhaa yake na ndiyo maana hata baada ya kupata ufadhili wa kufunguliwa
biashara tulijenga duka la mbao ambalo muda wowote linaweza kuondolewa kama
mwenye nyumba atahitaji tufanye hivyo.” Amesema Lidya
Kwa upande wake Mratibu wa mradi
wa kuwajengea uwezo watu wanaoishi kwenye kaya maskini na wenye ulemavu (DIG),
James Komba amesema Melea ni mmoja wa watu walionufaika na mradi huo kwenye
kundi la watu wenye ulemavu.
Amesema mradi huo uko kwenye kaya
300 ambazo zinaongozwa na wanawake pekee pamoja na watu wenye ulemavu lengo
likiwa ni kuwainua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi kutoka kwa ndugu
jamaa na marafiki.
Komba amesema wanufaika wa mradi
huo wamepewa mafunzo na kujengewa uwezo
wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kufungua maduka, kilimo, ufugaji wa
mbuzi, ng’ombe na nguruwe ambapo shirika
hilo limewawezesha wanufaika kwa kuwapatia wanyama wa kufuga pamoja na mitaji
ya kufungulia biashara zao.
“Baada ya kuwapa mitaji na
shughuli za kichumi hatujawaacha hivi hivi tumewakabidhi wa walimu wetu ambao
watawasimamia na kuwakagua kila mara lakini pia tumewakabidhi kwa mabwana
mifugo wa Halmashauri ambao watawapatia wanyama chanjo mbalimbali na hata
kuwatibu pale wanapoumwa lengo ni kuwawezesha wajitegemee na kuachana na
utegemezi waliokuwa nao,” amesema Komba.
Mwisho


Comments
Post a Comment