KIHENZILE AAGIZA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA MSALATO UKAMILIKE KWA WAKATI
Muhtasari: Mkandarasi anayejenga uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato ametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa uwanja huo ili ukamilike kwa wakati kwani ni mojawapo ya alama za kuonyesha kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameagiza mkandarasi anayejenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato uliopo Jijini Dodoma kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwani ni mojawapo ya alama zinazoonyesha kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi.
Kihenzile ametoa kauli hiyo leo alhamisi Julai 11, 2024 alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato uliopo Jijini Dodoma.
Amesema uwanja huo ni lango la utalii kwenye hifadhi mbalimbali za taifa ikiwemo Serengeti, Ruaha na maeneo mengine ya utalii kwa kuwa ni rahisi kufika kwenye maeneo hayo kutokea Dodoma.
“Mbali na reli ya mwendo kasi inayopita hapa, lakini pia uwanja huu ni alama mojawapo inayoonyesha dhamira ya serikali kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ambapo viongozi wa mataifa mbalimbali watakuwa wanatumia uwanja huu kuingia nchini badala ya kushukia Dar es Salaam na kupanda magari hadi huku,” amesema Kihenzile.
Amesema mradi huo upo nyuma kwa asilimia kidogo kwa sababu ya mvua zilizonyesha mwaka huu hivyo kusababisha baadhi ya kazi kutokamilika kwa wakati na kuwataka wakandarasi wanaojenga uwanja huo kuongeza kasi ili kufidia kazi ambazo hazijakamilika kabla mvua za masika hazijaanza kunyesha.
“Tunataka njia za kutua ndege zikamilke kabla ya mwezi April mwaka ujao na hata majengo ya uwanja yakamilike kabla ya Novemba mwaka 2025, kama mkataba unavyotaka,” amesema.
Akisoma taarifa ya mradi Kaimu Meneja wa wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Dodoma, Elisony Mweladzi amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye uwanja huo imefikia asilimia 67 wakati ulikuwa unatakiwa kufikia asilimia 70 mpaka wakati huu.
Aidha amesema ujenzi wa majengo umefikia asilimia 32.21 na wakati ilitakiwa kuwa asilimia 33.7 kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo mvua zilizokwamisha ujenzi huo kuendelea.
Naye Msimamizi wa mradi huo kutoka Tanroads, Mahona Luhende amesema ujenzi wa uwanja huo wa kimataifa ni wa miaka mitatu ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2025 ambapo utakapokamilika utahudumia jumla ya abiria 1.5 milioni kwa mwaka
Mwisho…..


Comments
Post a Comment