KATIBU MKUU CCT: VIJANA SIMAMIENI MIRADI YA MAENDELEO KWENYE MAENEO YENU

Muhtasari: Vijana nchini wametakiwa kufuatilia miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao kwa sababu inajengwa kwa kutumia kodi zao hivyo kama inajengwa kwa kusuasua au chini ya kiwango ni lazima wachukue hatua za kuwawajibisha waliowapa dhamana ya kusimamia miradi hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Dk Moses Matonya amewataka wananchi kukagua miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kujua kama inatekelezwa kwa ubora na kiwango kinachotakiwa kwa sababu inajengwa kwa kutumia kodi zao.

Dk Matonya ametoa kauli hiyo leo jumatano julai 10, 2024 wakati akizungumza na vijana kwenye semina iliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya mtandao wa madeni na maendeleo (TCDD) Jijini Dodoma.

Amesema serikali inatekeleza miradi mingi kuanzia ngazi ya vijiji, kata, Halmashauri hadi serikali kuu lakini vijana hawaijui miradi hiyo wala utekelezaji wake kwa sababu wanadhani ni mambo ambayo hayawahusu, na kuwataka kufuatilia miradi hiyo kwa sababu ni kodi zao.


Katibu mkuu wa jumuiya ya kikristo Tanzania (CCT) Dk Moses Matonya (aliyesimama) akizungumza na vijana kwenye semina ya kuwajengea uwezo kuhusu deni la Taifa iliyoandaliwa na matandao wa madeni na maendeleo (TCDD) Jijini Dodoma Leo Jumatano Julai 10, 2024 


Amesema miradi mingi inatekelezwa chini ya kiwango na inagundulika siku viongozi wa kitaifa wakiitembelea na wakati wananchi wa eneo hilo wapo na wanaona kila kinachoendelea lakini hawafutilii miradi hiyo na kuwataka wabadilike na waanze kufuatilia miradi yote kwenye maeneo yao kwa sababu ni mali yao kama Watanzania.

“Kama ni shule au zahanati inajengwa ni lazima mfuatilie na mjue ni kiasi gani cha pesa kimetolewa kwenye mradi huo, mfuatilie pia mjue kama ujenzi unaoendelea una thamani sawa na kiwango kilichotolewa msikae kimya na kama mnaona kuna makosa yanafanyika toeni taarifa ili hatua zichukuliwe,” amesema Dk Matonya.

Aidha amewataka vijana kuhudhuria kwenye mikutano inayoitishwa na viongozi wa serikali za mitaa kwa sababu huko ndipo hutolewa taarifa za miradi mbalimbali inayoendelea kwenye mtaa husika.

“Msiwaache wanasiasa kuendesha kila kitu kwenye maisha yenu nendeni mkafanye siasa za maendeleo siyo lazima mkagombee kwenye vyama vya siasa bali mnaweza kufanya ushawishi kwenye jamii yenu na kujiletea maendeleo hata bila kugombea uongozi,” amesema Dk Matonya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa TCDD, Hebron Mwakagenda amewataka vijana hao kufuatilia kwa makini bajeti ya serikali inaposomwa kwani inawahusu.


Mkurugenzi wa mtandao wa madeni na maendeleo (TCDD) Hebron Mwakagenda (aliyesimama) akizungumza kwenye semina ya kuwajengea uwezo vijana kuhusu deni la Taifa Jijini Dodoma


Amesema deni la Taifa linaloongezeka kila mwaka kwenye bajeti ya Taifa linawaathiri vijana kwa sababu linagusa maisha yao ya kila siku ikiwemo afya, elimu na huduma zote za kijamii hivyo litawaathiri siku za usoni watakapokuja kushika madaraka.

Tumaini Kivuyo ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Tumaini Foundation amesema vijana wanatakiwa kujengewa uwezo ili waweze kusimamia miradi iliyopo kwenye maeneo yao kwa sababu wengi hawajui kama inawahusu.

Amesema kuna mambo mbalimbali yanayoendelea nchini vijana wamenyamaza bila kujua kuwa yatawaathiri kwa siku za usoni na kuwataka kuamka na kuanza kupaza sauti zao hasa wanapoona mabo hayaendi sawa.


Baadhi ya vijana walioshiriki kwenye semina ya kujengewa uwezo kuhusu deni la Taifa iliyoandaliwa na mtandao wa madeni na maendeleo (TCDD) Jijini Dodoma


Naye Emeran Riziki kutoka taasisi ya Education Stars in the Universe (ESITU) amesema ni wakati sasa wa kuwatengeneza vijana ili wawe viongozi wazuri baadaye kwa kuwashirikisha masuala muhimu yanayoendelea nchini badala ya kuwaacha na kujiona si sehemu ya mabadiliko yanayoendelea nchini.

Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI