ESWATIN YAJA KUJIFUNZA NAMNA YA KUENDESHA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII PSSSF

Muhtasari: Ujumbe wa watu tisa kutoka nchini Eswatin wametembelea mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF ili kujifunza namna bora ya uendeshaji wa mifuko ya pensheni na kuachana na mfuko wa akiba ambao bado unatumika nchini humo.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema kuwa itapeleka wataalam wa kuendesha mifuko ya hifadhi za jamii kutoka mfuko wa PSSSF nchini Eswatin ili kuwafundisha namna kuanzisha mfuko wa hifadhi ya jamii unaotoa pensheni kwa wanachama wake na kuachana na mfuko wa akiba ambao unatumika nchini humo kwa sasa.

Hayo yamesema leo ijumaa Julai 19, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF Abdul-Razaq Badru baada ya kupokea ujumbe wa viongozi tisa akiwemo waziri wa utumishi wa umma kutoka nchini Eswatin kwa ajili ya ziara ya kuja kujifunza uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii inayotoa pensheni kwa wanachama wake.

Badru amesema nchi ya Eswatin bado inatumia mfuko wa akiba kwa wanachama wake na wanataka kuanza kutoa pensheni hivyo wamekuja kujifunza namna ya kuendesha mifuko hiyo nchini ili wakaanze kuitumia nchini kwao.


Waziri wa Utumishi wa Umma kutoka nchini Eswatin, Mabulala Maseko (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi mkuu wa mfuko wa hifadhi ya jamii (PSSSF) Abdul-Razaq Badru Leo jumamosi Julai 20, 2024 alipotembelea mfuko huo ili kujifunza namna ya kuendesha mifuko ya hifadhi za jamii Jijini Dodoma 


“Hii ni fahari kwetu kuona nchi nyingine zinakuja kujifunza namna ya kuendesha mifuko ya hifadhi za jamii nchini kwetu, na kwa sababu wametuchagua kuwaelekeza namna ya kuendesha mifuko hii tutawapa wataalam ambao watawasaidia kuanzisha mfumo wa kuwalipa wanachama wao pensheni mpaka watakapoweza kujisimamia wenyewe,” amesema Badru.

Amesema ziara hiyo ya mafunzo inaonyesha ni jinsi gani PSSSF inaendesha mfuko huo kwa mafanikio kwa kuwalipa wanachama wake mafao kwa wakati pamoja na kuwekeza vitega uchumi mbalimbali kwa ajili ya kuongeza kipato kwa ajili ya wanachama wao.

Amesema Eswatin imeonyesha shauku kubwa ya kujifunza mbinu bora za uendeshaji wa mfuko, mifumo ya malipo yenye ufanisi na namna ya kuongeza thamani kwa wanachama wao.

Kwa upande wake Waziri wa utumishi wa Umma kutoka nchini Eswatin, Mabulala Maseko amesema wametembelea nchi nyingi kwa ajili ya kujifunza namna ya kuendesha mifuko ya hifadhi za jamii inayotoa pensheni kwa wanachama wao na kuona kuwa PSSSF ina mafanikio makubwa kuliko nchi nyingine.

Amesema baada ya mafunzo hayo watakwenda kuanzisha mfumo huo wa kutoa mafao kwa njia ya pensheni kwa watumishi wote wa umma na sekta binafsi kwa kuwa wameona mfumo huo ni bora kuliko mfumo wa akiba ambao wanautumia sasa.

Amesema wameelezwa namna ya kusimamia shughuli za uwekezaji kuhakikisha kwamba wanapowekeza mitaji ya mifuko ielekezwe maeneo yenye tija na yanayozalisha  ili uwekezaji uwe na mchango katika maendeleo na uchumi wa nchi.

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI