Ndoa za utotoni zinazima ndoto za wasichana
Muhtasari: Shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative limeitaka serikali kuharakisha muswada wa mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwani imekuwa chanzo cha wasichana wengi kuolewa ndoa za utotoni chini ya miaka 18 na wazazi kujificha kwenye kichaka cha sheria hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Msichana Initiative ambalo linajishughulisha na mapambano ya ukatili dhidi ya wasichana nchini limeitaka serikali kuharakisha muswada wa mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwani imekuwa chanzo cha wasichana wengi kuolewa ndoa za utotoni chini ya miaka 18 na wazazi kujificha kwenye kichaka cha sheria hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa kitaifa majukwaa ya wanajamii Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Rebeca Gyumi amesema shirtika la msichana Initiative limekuwa ni moja ya mashirika vinara nchini kupambania mabadiliko ya sheria ya ndoa.
Amesema kutokana na mkanganyiko wa umri wa kuolewa mtoto wa kike shirika hilo lilipeleka kesi mahakamani ya kuomba sheria ya ndoa ipewe tafsiri ambapo uamuzi uliotolewa na mahakama ya rufaa mwaka 2019
Mkurugenzi huyo amesema kazi wanazofanya na wanajamii zinaendelea kuthibitisha kwamba sheria hiyo bado ni kikwazo kwa sababu mara nyingi kesi wanazokutana nazo kama mzazi kaamua kumuoza mtoto kunakuwa na viashiria vya kumtoa kwenye mfumo wa shule au mtoto alimbiwa ajifelishe ili aonekane kuwa hayupo kwenye mfumo wa shule kwa sababu hawezi kulindwa tena na sheria zilizopo.
“Maana yake sheria ya ndoa inakuwa inatoa huo mwanya wa mtoto kuozwa akiwa na umri wa miaka 14 kwa hiyo kazi ambayo tunafanya sasa hivi imekuwa ni kuendelea kuishinikiza serikali kuleta muswada wa mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na tuliona wiki iliyopita Naibu Waziri wa Katiba na Sheria alisema kwamba sheria hiyo au muswada huo upo tayari,” amesema Mkurugernzi huyo na kuongeza kuwa,
“Kwa hiyo nitumie jukwaa hili kusema kwamba tunatamani kuona serikali inafanyia kazi haiwi ni ahadi kila mwaka kwamba wataleta muswada wataleta muswada kwa sababu nyuma ya hii sheria kuna maisha halisi ya wasichana ambayo yanaathirika na yanakatishwa kwa sababu sheria hii ya ndoa bado ipo na inanyima na inakata nafasi yao ya kujiamulia kuhusu maisha yao na kutimiza ndoto zao.”
Ameisihi serikali kuona uharaka wa kuleta muswada huu ili sheria ya ndoa ibadilike kwani kesi kuhusu ndoa za utotoni zimekuwa ni nyingi na hazifiki mwisho kutokana na sheria hiyo ya ndoa ambayo bado inatumika mpaka sasa.
Amesema tangu waanze kampeni hiyo ya kupinga ndoa za utotoni wamepokea zaidi ya kesi 300 za watoto kuozeshwa katika umri mdogo lakini hakuna mwendelezo wa kesi wala hukumu kwa kuwa wazazi wanasimamia sheria ya ndoa iliyopo hata kama mtoto alikuwa ni mwanafunzi.
Mwenyekiti wa jukwaa la wanajamii kutoka Wilayani Nzega, Lucia Nzige amesema mila tamaduni na desturi zinakwamisha mapambano dhidi ya ukatili wa wasichana hasa kwenye suala la ndoa kawani wazazi wanachoangali ni kiasi cha mali wanachopata kwa kumuozesha mtoto wao bila kujali kama wanakatisha ndoto zake.
Amesema mikoa wa Tabora na Dodoma kiwango cha ndoa za utotoni kipo juu ukilinganisha na mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ambapo napo kuna ukatili mwingine wa ubakaji na vipigo kwa wasichana.
Amesema ni jukumu la jamii kuhakikisha hakuna ukatili unaofanyika kwenye maeneo yao ili watoto wa kike waweze kumaliza masomo yao na kutimiza ndoto zao bila kikwazo chochote.
Naye mwenyekiti wa jukwaa la wanajamii kutoka Wilayani Kongwa Onesmo Semundu amesema elimu inayotolewa kuhusu ukatili kwa wasichana imeanza kuzaa matunda kwa kupunguza matukio ya ukatili kwenye jamii japo sheria ya ndoa yam waka 1971 imeendelea kuwa kikwazo katika mapambano hayo.
Amesema wazazi na walezi wanawakatisha masomo watoto wao wa kike ili wakaolewe na wale ambao watakataa kuacha shule wanalazimishwa kufanya vibaya kwenye mitihani ya taifa ili wasifaulu ili waende wakaolewe na wazazi wao wapate mali.
Amesema ifike hatua sasa serikali iifanyie marekebisho sheria hiyo ya ndoa ili ijulikane mtoto ni nani kwani bado kuna shida kwenye tafsiri ya mtoto kwani chini ya miaka 18 anahesabiwa kuwa bado ni mtoto lakini sheria ya ndoa inaruhusu aolewe akiwa na umri wa miaka 14.



Comments
Post a Comment