WATU WENYE UALBINO WALIA NA WAGANGA WA KIENYEJI NA UCHAGUZI MKUU
Muhtasari: Waganga wa kienyeji na suala la uchaguzi mkuu vimetajwa kuwa haviwezi kukwepa lawama za ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani kila kinapofika kipindi cha uchaguzi ndipo ukatili huo hutokea na waganga wa kienyeji wakitajwa kuwa ndiyo chanzo cha ukatili huo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Taasisi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ya Foundation for disabilities hope (FDH) imesema kuwa waganga wa kienyeji na suala la uchaguzi mkuu hawawezi kukwepa lawama za ukatili wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani kila yanapotokea mauaji ya watu hao ni lazima watajwe.
kauli hiyo imetolewa Leo jumatatu Juni 24, 2024 na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Michael Salali wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio ya kujeruhiwa na kuuawa kwa watu wenye ualbino nchini Jijini Dodoma.
Salali amesema Taasisi hiyo inalaani tukio la kujeruhiwa kwa mtoto Julius Kazungu (10) mkazi wa Mkoani Geita na watu wasiojulikana pamoja na kutekwa na kisha kuuawa kwa mtoto Asimwe Novath (2) ambaye alinyofolewa baadhi ya viungo vyake na kutupa kwenye karavati ambapo watoto wote wawili ni wenye ualbino.
Amesema kwenye matukio hayo ya ukatili dhidi yao waganga wa kienyeji na suala la uchaguzi haviwezi kukwepeka kwani kila yanapotokea matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino ni lazima watu hao watajwe.
Mkurugenzi wa Taasisi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Foundation for disabilities Hope (FDH), Michael Salali"Mtaniuliza kwanini tunahusisha ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na uchaguzi mkuu hili halikwepeki kwa sababu kila ikifika kipindi hiki ndipo huwa tunashuhudia ukatili ukiongezeka na wakati miaka mingine ambayo haina uchaguzi hakuna matukio kama hayo lakini pia kwenye kila tukio wanaokamatwa kuhusika hapakosi mganga wa kienyeji ambaye huwa ndiyo chanzo cha ukatili huo," amesema Salali.
Amesema kikifika kipindi cha uchaguzi watu wenye ualbino huwa wanaishi kwa hofu na mashaka kwa kuhofia maisha yao kwani huwa hawajui watu waliowazunguka wanawawazia nini.
Amesema lakini mwaka huu mauaji ya Asimwe yamechukua sura mpya kwani hadi kiongozi wa dini amehusika hivyo kuwafanya watu wenye ualbino kuishi kwa hofu zaidi wasijue ni nani wa kumwamini.
Amesema jamii hiyo bado ina imani na serikali na kuwataka viongozi wote kuanzia ngazi za chini kufuata maelekezo yaliyotolewa na waziri Mkuu ili kuwalinda watu wenye ualbino .
Amesema maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu kuhusu kuwalinda watu wenye ulemavu ikiwemo mpango mkakati wa kuwalinda yakifuatwa vizuri yatakuwa mwarobaini wa matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino nchini.
Wakati Mkurugenzi huyo akiyasema hayo, Umoja wa waganga na wakunga wa tiba za asili Tanzania (Uwawata) wamekana kumtambua mtu aliyetajwa na jeshi la polisi kuwa ni mganga wa kienyeji na kwamba hajasajiliwa na Umoja huo.
Katibu Mkuu wa Uwawata, Lucasi Mlipu amesema Umoja huo unafanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi hivyo watu wanaojiita waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi si wanachama wao bali ni matapeli.
Mlipu alienda mbali zaidi na kusema kuwa hakuna kiungo cha binadamu kinachotumika kwenye tiba asili hivyo wote wanaofanya hivyo ni matapeli ambao wanaojiita waganga wa kienyeji ili kuwaharibia sifa yao.
Naye Katibu wa Uwawata Mkoa wa Kagera Patian Kashubi amesema zipo sifa za mtu kuitwa mganga wa kienyeji ikiwemo kurithishwa na mizimu au mababu lakini waganga wa siku hizi hawana hizo sifa na wanajiita waganga na kuanza kuwatapeli watu.
Kuhusu mauaji ya watu wenye ualbino kuhusishwa na uchaguzi mkuu Kashubi amesema kiongozi yeyote anayetaka kuingia madarakani kwa kutoa kafara watu wenye ulemavu hafai kuwa kiongozi kwani anajijua kuwa hana sifa za kuongoza na ndiyo maana anataka kuingia kwa njia zisizo halali.
Mwisho

Comments
Post a Comment