WATOTO WAPAZA SAUTI KUHUSU KUFANYIWA VITENDO VYA UKATILI
Muhtasari: Kwa mujibu wa takwimu za Wilaya cha Chamwino za Oktoba 2023 hadi Juni 2024 kesi za ukatili zilizoripotiwa kituo cha polisi Chamwino zilikuwa 118 kati ya hizo wanaume 109, wanawake 9, watoto 26, kesi 88 zipo mahakamani, 32 wameshawatiwa hatiani kwa matukio ya ubakaji, ukeketaji na vipigo.
Na Mwandishi Wetu, Chamwino
BARAZA la ulinzi wa mtoto wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma limeitaka serikali kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha sera na sheria ya ulinzi wa watoto ikiwamo sheria ya ndoa yam waka 1971 inayoruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 kuolewa ili kutokomeza ukatili dhidi yao.
Wito huo umetolea leo Ijumaa Juni 21, 2024 na mwenyekiti wa Baraza hilo Anthony Mlewa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliofanyika katika Kijiji cha Kawawa kata ya Msanga wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Actionaid Tanzania yenye kauli mbiu; elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi.
Mlewa amesema ili kudhibiti ukatili unaoendelea dhidi ya watoto, jitihada za wadau wote na serikali ni muhimu kwa maendeleo endelevu.
Mbali na hayo baraza hilo limewaomba wanajamii kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa dhidi ya ukatili kwa watoto.
Amesema miongoni mwa changamoto inazowakabili ni ushirikishwaji duni kwenye masuala mbalimbali yanayohusu watoto na maamuzi , ukiukwaji wa haki za watoto na uhaba wa miundombinu mashuleni nakutaka iboreshwe.
“Mimba za utotoni, ndoa za utotoni, vipigo vilivyopitiliza bado ni tatizo, pale penye haki wazazi wanawajibu wa kuhakikisha ulinzi wa mtoto ni kipaumbele sio ombi, lakini pia wazazi wanawajibika kwenye masuala ya maadili kwa watoto,’’ amesema Mlewa.
Naye mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo Mratibu msaidizi wa polisi Yusuph Abdallah amesema kwa mujibu wa takwimu za Wilaya cha Chamwino za Oktoba 2023 hadi Juni 2024 kesi za ukatili zilizoripotiwa kituo cha polisi Chamwino zilikuwa 118 kati ya hizo wanaume 109, wanawake 9, watoto 26, kesi 88 zipo mahakamani, 32 wameshawatiwa hatiani, miongoni mwa kesi hizo ni pamoja na ubakaji, ukeketaji na vipigo.
‘’Ulezi wa watoto unategemea pande kuu tatu, wazazi, walimu na wanajamii, wazazi tuwe karibu na watoto ili kujua mahitaji yao,’’ amesema Abdallah
Abdallah amewataka wazazi kutoa taarifa kwa dawati la jinsia endapo watapata taarifa za ukiukwaji wa haki za bindamu.
Kwa upande wake Ofisa ustawi wa jamii wilaya ya Chamwino Obed Fredy amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwaachia watoto simu kwa muda mrefu ili kupunguza mmomonyoko wa maadili.
‘’Watoto wanajifunza matendo maovu kupitia mitandao ya kijamii hivyo niwaase wazazi kuwapeleka kwenye nyumba za ibada ikiwemo misikitini na makanisani ili waweze kujifunza maadili mema,’’ amesema Fredy na kuongeza kuwa,
“Maarifa yamepungua kutokana na utandawazi, vijana wanashinda kwenye kubeti, niwatake wazazi tutenge muda wa kufuatilia malezi ya watoto wetu kwa kuwa wanajifunza kutoka kwetu, mambo yetu na matendo yetu yanachangia kuathiri watoto wetu tuache.’’
Amewataka wazazi wazingatie maadili kwani utandawazi umeleta madhara makubwa hasa kwa watoto wadogo hivyo wapunguze kuwapa watoto simu maana huko ndiko wanakojifunza vitendo viovu kupitia mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti wa jukwaa la wakulima wadogo wilaya ya chamwino (JUWACHA) lililopo chini ya shirika lisilo la kiserikali la Actionaid Tanzania Janeth Nyamayahasi amewataka wazazi kutenga muda kwa ajili ya malezi ya watoto kwa kushirikiana na viongozi wa dini , wazee wa kimila ili kupambana na mmomonyoko wa maadili.
Clezensia Sahani kutoka shirika la Actionaid Tanzania amesema lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za watoto ikiwa ni pamoja kupinga ukatili dhidi yao
“Lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu hata kama ni mlemavu, ukiangalia saivi kuna mmomonyoko wa maadili watoto wanajifunza kwa wazazi maana utandawazi unawaharibu, elimu wanayoipata iendane na maadili ya kitanzania,’’ amesema Sahani
Mwisho


Comments
Post a Comment