WACHIMBAJI WADOGO WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA ZA KISASA KUCHENJUA MADINI BADALA YA KUTUMIA KEMIKALI YA ZEBAKI
Muhtasari:
Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya
kemikali ya zebaki inayotumika kwenye uchenjuaji wa madini ili kulinda afya zao
na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya kemikali hiyo ikiwemo magonjwa ya
ngozi, figo, kifua na hata kifo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini wametakiwa
kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali ya zebaki inayotumika kuchenjulia madini
ili wajiepushe na madhara yanayotokana na matumizi holela ya kemikali hiyo
ikiwemo magonjwa ya ngozi, figo, saratani, kifua na hata kifo.
Ushauri huo
umetolewa leo jumamosi Juni 22, 2024 na Baraza la Taifa la usimamizi wa
mazingira (NEMC) na Ofisi ya Mamlaka ya maabara
ya mkemia mkuu wa serikali wakati wakitoa semina ya matumizi sahihi ya kemikali
ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini waliokutana Jijini Dodoma.
Akizungumza
kwenye mafunzo hayo Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo (EHPMP), Dk Betrina Igulu amesema wachimbaji wadogo wengi hawana uelewa wa
madhara ya kemikali ya Zebaki na ndiyo maana wengi wao wameathirika na matumizi
ya kemikali hiyo bila kujua.
Amesema
wengi wao wanatumia kemikali hiyo bila kuchukua tahadhari zozote za kiusalama
kama vile kuvaa mavazi yanayowakinga kugusana na kemikali hiyo, kuvaa glove
mikononi, barakoa na mabuti na hivyo kujikuta wanaathirika na kemikali hiyo
baada ya kipindi cha muda mrefu.
“Serikali
haijapiga marufuku matumizi ya zebaki kwenye migodi lakini inatakiwa itumike kwa
tahadhari kubwa na kwa kiwango kidogo ili isilete madhara kwenye afya zenu, kwa
sababu unaweza ukadhani kuwa unatafuta fedha lakini hata ukiipata usiitumie kwa
raha kwa sababu unakuwa na magonjwa yanayotokana na kemikali hiyo,” amesema Dk
Igulu na kuongeza kuwa,
“Pia mnatakiwa
kutumia zebaki kulingana na kiwango kilichoidhinishwa na shirika la afya
duniani cha asilimia 15 tu kwani tulifanya utafiti kwa kushirikiana na Wizara
ya afya kwa wachimbaji wadogo wa Mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Mbeya na
Singida ambapo tuligundua kuna matumizi makubwa ya kemikali ya zebaki hadi
asilimia 60 na baadhi ya watu wameshapata magonjwa yanayotokana na kemikali
hiyo.”
Amesema Nemc
ina wajibu wa kulinda sheria ya mazingira ili kuhakikisha kuwa hakuna uharibifu
wowote unaotokana na matumizi ya kemikali kwenye migodi ya wachimbaji wadogo na
kwamba atakayebainika kuvunja sheria atafutiwa leseni yake ya uchimbaji.
Amewataka
wachimbaji hao kuhifadhi kwa usalama mabwawa yanayohifadhi maji yenye kemikali
ili yasilete madhara kwenye mazingira na kwenye vyanzo vya maji kwani ni hatari
kwa viumbe hai.
Kwa upande
wake Meneja wa kanda ya kati kutoka Ofisi ya mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu
wa serikali, Gerald Mollel amewataka wachimbaji hao kuhifadhi na kutumia kwa
usahihi kemikali zote zinazotumika migodini.
Aidha
amesema matumizi mabaya ya kemikali hizo ni hatari kwa afya zao kwani madhara
hayataonekana haraka lakini baada ya miaka 10 ndipo yatakapoanza kuonekana
ikiwemo kutetemeka mikono, miguu na kichwa, ngozi kubabuka, saratani na hata kifo.
Amesema hata
kama wanatafuta fedha lakini wachukue tahadhari ya kulinda afya zao ili fedha
watakazozipata waweze kuzitumia kwenye malengo waliyoyakusudia badala ya
kutumika kujiuguza.
“Kuna
kemikali nyingine hazihitaji kugusa moto hivyo unapozitumia ni lazima usivute
sigara kwani kwa kufanya hivyo utaweza kutengeneza bomu ambalo litawaathiri
watu wengi bila wewe kujua hivyo kabla ya kutumia kemikali hakikisha unasoma
maelekezo ya matumizi yake na namna bora ya kuzihifadhi ili zisilete madhara,” amesema
Mollel
Baadhi ya
wachimbaji hao wameiomba serikali kuwaletea teknolojia mbadala ya kuchenjua
madini yao badala ya kemikali ya zebaki kwani hata wakiitumia wanapata asilimia
55 tu madini wanayoyataka badala ya kuyapata yote.
Martha
Mwageni amesema kama kemikali zinazotumika kwenye migodi zina madhara wanaomba
serikali iwapelekee mitambo yenye teknolojia ya kisasa itakayowawezesha
kuboresha kazi zao badala ya kuhatarisha afya zao kwa kutumia kemikali zenye
sumu.
Amesema
wachimbaji wengi wadogo wanatumia kemikali ya zebaki kwa kuwa ni rahisi
kupatikana na kwa gharama nafuu bila kujali athari za kiafya zitakazowapata.
Naye Dk
Mzeru Nibuka amewataka wamiliki wa migodi kuweka sheria ya kuwazuia watu
waliolewa kufanya kazi kwenye migodi yao kwani huwa hawachukui tahadhari zozote
za kiafya.
Amesema kama
mtu anataka kulewa alewe baada ya kazi na si wakati wa kazi kwani hao ndiyo
huwa hawavai vitendea kazi vya kuwakinga na kemikali za zebaki na mwisho wa
siku ndiyo huwa wanaumwa na kuumia zaidi huko migodini wakati ndiyo nguvu kazi
inayotegemewa.
Mwisho.


Comments
Post a Comment