VITA DHIDI YA VIMELEA SUGU VYA DAWA YATINGA BUNGENI
Muhtasari: Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. wamezindua umoja wao wa kukabiliana na usugu wa vimelea vya dawa (uvida) nchini ambapo wameahidi kutunga sheria na sera zitakazomaliza tatizo hilo nchini ambalo linakuwa kwa Kasi.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni vinara wa kupinga usugu wa vimelea vya dawa (uvida) wamesema kuwa watasimamia utungwaji wa sera na sheria nchini zitakazowezesha kumaliza tatizo hilo ambalo limetajwa na Shirika la afya Duniani kama janga linaloikabili jamii kwa sasa.
Kauli hiyo imetolewa leo alhamisi Juni 20, 2024 na Mwenyekiti wa umoja huo Dkt Hamis Kigwangala wakati wa uzinduzi wa umoja huo uliofanywa na Shirika la One Healthy Society Jijini Dodoma.
Dkt Kigwangala amesema imefika wakati sasa wa kutunga sheria na sera zitakazomaliza tatizo hilo la usugu wa vimelea vya dawa kwani likiachwa likaendelea litasababisha madhara makubwa ikiwemo vifo na kuporomoka kwa uchumi.
"Niahidi sisi kama wabunge vinara wa kupinga usugu wa vimelea vya dawa tutahakikusha kuwa tunatunga sheria na sera nzuri ambazo zitamaliza tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau wote wa sekta ya afya kwani hali siyo nzuri kwa sasa," amesema Dkt Kigwangala.
Aidha amesema ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa watu wake wanapata huduma nzuri hasa za maji ya kunywa ili kupunguza uwezekano wa kupunguza maambukizi na kuwakinga wasipate magonjwa ambayo yatapelekea usugu wa vimelea vya dawa.
Aidha ameiasa jamii kuzingatia matumizi sahihi ya dawa wanazotumia ili kujiepusha na usugu wa vimelea ambalo ni tatizo kubwa linaloinyemelea Dunia kwa sasa.
"Dawa ikishaweka usugu ili kuipata dawa nyingine mbadala ya kupambana na ugonjwa huo inachukua takribani miaa 20 Sasa piga hesabu hapo katikati tutakuwa tumewapoteza watu wangapi kutokana na usugu wa vimelea vya dawa, hivyo tunatakiwa tuanze kuchukua hatua sasa ili kukabiliana na tatizo hili," amesema Dkt Kigwangala
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bunge Dkt Joseph Mhagama ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson kwenye uzinduzi wa umoja huo amesema ni kweli kwamba tatizo la usugu wa vimelea vya dawa lipo hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuliokoa Taifa na janga hilo.
Amesema wabunge waliochaguliwa kukabiliana na uvida ni wabobezi kwenye masuala ya afya hivyo jukumu lao kitakuwa jepesi ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosha kuhusu suala hilo.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la One Healthy Society, Hamisi Msagama amesema wameamua kulileta suala la uvida kwa watunga sera na sheria ili lipate msukumo wa kutosha katika mapambano yake.
Amesema kwa muda mrefu suala hilo lilikuwa mikononi mwa madaktari na wanasayansi lakini kwa sasa wameamua kuwashirikisha wabunge ili vita hiyo ipate mwitikio mkubwa kwani wanawawakilisha wananchi wa hali ya chini ambao pia ni waathirika wa uvida.
Msagama amesema kwa mujibu wa Shirika la afya Duniani (WHO) takribani watu milioni 10 watakuwa na usugu wa vimelea vya dawa ifikapo mwaka 2050 ambapo takwimu zisizo rasmi zinaonyesha mwaka 2018 watu 700,000 Duniani kote walikuwa na uvida.
Mwisho....


Comments
Post a Comment