TLS: SHERIA YA UHURU WA KUJIELEZA IENDANE NA MABADILIKO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Muhtasari: Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimesema ili sheria ya uhuru wa kujieleza ifanye kazi vizuri kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha katiba namba 18 ni lazima katiba ifanyiwe marekebisho upya ili kifungu hicho kiendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo hivi sasa ambayo yanaafanya baadhi ya mipaka ya kujieleza iliyopo kwenye katiba kushindwa kutekelezeka.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAKAMU wa Rais wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) Deus Nyabiri amesema upo ulazima wa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi ili iendane na sayansi na teknolojia ya sasa hasa kwenye kifungu cha uhuru wa kujieleza.
Nyabiri ametoa wito huo leo jumanne Juni 25, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo mawakili kuhusu uhuru wa kujieleza Jijini Dodoma.
Mwanasheria huyo mwandamizi amesema kila mtu Duniani ana uhuru wa kujieleza tangu anapozaliwa na hata katiba ya nchi imelieleza hilo lakini kwa sasa kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kuna haja ya kufanyia marekebisho sheria inayohusu uhuru huo na hata ikibidi katiba yote.
Makamu wa Rais wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) Deus Nyabiri (aliyesimama) akizungumza na mawakili wanaopatiwa mafunzo ya sheria ya uhuru wa kujieleza Jijini Dodoma
"Katiba imeeleza vizuri kuhusu uhuru wa kujieleza lakini pia imeeleza mipaka ya uhuru huo kuwa usivunje sheria za nchi lakini kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo ambayo yanavunja mipaka iliyowekwa kwenye katiba kuna haja ya kuangalia upya vifungu vya katiba pamoja na sheria zilizopo," amesema Nyabiri.
Amesema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo Duniani kila mtu anatumia uhuru wa kujieleza kwenye mitandao ya kijamii kama anavyotaka bila kujali kama anavuka mipaka iliyowekwa au la au hata kama anawaudhi watu wengine kuhusu uhuru huo.
"Sasa hivi tunashuhudia kwenye mitandao ya kijamii watu wanakuta ajali imetolea, badala ya kutoa msaada kwa majeruhi yeye anapiga picha za marehemu na kuanza kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii bila kujua kuwa anawakera watu wengine ambao hawapendi kuona picha za aina hiyo, hivyo kuna haja ya kuliangalia hili kwenye katiba na sheria za nchi," amesema Nyabiri.
Amesema hata sheria ya makosa ya mtandaoni iliyopo inawabana wale ambao wanatumia mitandao ya kijamii vibaya na kuwaachia wale ambao wanatumia uhuru wao wa kujieleza kwa kuwadhalilisha wengine mitaani bila kutumia mitandao na kutaka sheria hiyo sasa iwabane watu wote bila kujali wanatumia mitandao au la.
Kwa upande wake wakili Esta Safari kutoka Mkoani Mwanza amesema hata wateja wanaowahudumia hawajui mipaka ya kujieleza inaishia wapi kwani wengi wao ni wale ambao wanatumia mitandao ya kijamii kuelezea fikra zao.
Amesema wengi hawajui kama kuelezea fikra zako mitandaoni kunaweza kuleta taharuki kwa watu wengine kwa kuvunja amani au kuhatarisha usalama wa nchi hivyo huwa wanajikuta wakiangukia kwenye vyombo vya sheria bila kujua.
"Ili hili suala la uhuru wa kujieleza likae vizuri ni lazima mabadiliko yaanzie kwenye katiba na sheria zilizopo kwani watu wengi wanajikuta wamevunja mipaka bila kujua hasa kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kudhani kuwa ni haki yao kumbe kuna mipaka ambayo hawapaswi kuvuka hata kama wanajieleza," amesema Esta.
Naye wakili wa kujitegemea Ferdinand Makore amesema japo katiba imeeleza kuwa kila mtu ana uhuru wa kujieleza na kuweka mipaka ya uhuru huo lakini kuna haja ya kuangalia upya mipaka hiyo kutokana na mageuzi ya teknolojia iliyopo sasa.
Amesema watu wengi hujikuta kwenye vyombo vya sheria bila kujua kwa yale wanayoyachapisha kwenye mitandao ya kijamii wakidhani ni maoni yao binafsi kumbe wanakuwa wamevunja katiba ya nchi.
Mwisho...
Makamu wa Rais wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) Deus Nyabiri


Comments
Post a Comment