Kituo cha kwanza cha taarifa za mapema za majanga Barani Afrika kimezinduliwa Tanzania
Muhtasari: Serikali imezindua chumba cha taarifa za tahadhari za mapema za majanga ambacho kitaiwezesha serikali kuchukua hatua mapema za majanga kabla hayajatokea nchini.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge Sera na Uratibu, Jenista Mhagama amezindua chumba cha taarifa za tahadhari ya mapema kuhusu majanga nchini kitakachowezesha serikali kuchukua hatua za haraka kabla majanga hayo hayajatokea.
Kituo hicho ambacho ni cha kwanza kujengwa Barani Afrika kimezinduliwa leo ijumaa Julai 14, 2024 Jijini Dodoma ambapo kimejengwa kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo la nchini Italia (AICS) ambacho kitakuwa na mfumo utakaowezesha kufuatilia, kuchambua na kuratibu taarifa na takwimu za majanga, hali ya uwezekano wa kuathirika, utabiri wa hali ya hewa na haidrolojia hatarishi na uchambuzi wa madhara yanayoweza kutokea.
Mhagama amesema chumba hicho kitasaidia serikali kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya mvua kubwa za el nino, mafuriko, ukame, vimbunga na magonjwa ya mlipuko.
Amesema hilo linawezekana kwani mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini (TMA) ilitoa tahadhari ya mvua za el nino tangu Julai mwaka 2023 kwa mikoa 14 ambayo ilikumbwa na mvua hizo na ndiyo maana madhara yaliyopatikana si makubwa kulinganisha na hali ilivyokuwa.
“Mamlaka ya hali ya hewa ilikaa na ofisi ya Waziri Mkuu tangu Julai mwaka 2023 na kutueleza kuwa kutakuwa na mvua kubwa za el nino na kwa bahati nzuri tuliitumia taarifa hiyo na kuchukua tahadhari kwenye wilaya za mikoa yote 14 iliyokubwa na mvua hizo na ndiyo maana madhara hayakuwa makubwa sana,” amesema Mhagama.
Amesema hiyo inatokana na uboreshwaji wa mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini (TMA) ambayo kwa sasa imekuwa ikitoa tarifa za uhakika kwa asilimia 95 juu ya uwepo wa mvua kubwa na vimbunga ambavyo vimeshuhudiwa kwa siku za hivi karibuni.
“Sasa hivi TMA ikitangaza kutakuwa na mvua kwa siku tatu mfululizo ujue ni kweli mvua itakuwepo hivyo jiandae na miamvuli na walituambia kuwa itakapofika mwezi Juni mwaka huu hali itakuwa shwari na kweli tunashuhudia kwa sasa hali imetulia hivyo kituo hiki ni muhimu sana kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya asili,” amesema Mhagama.
Amesema majukumu ya kituo hicho ni kufuatilia mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira itakayowezesha kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema na hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili janga husika.
Aidha amesema jukumu lingine ni kusambaza taarifa za tahadhari ya mapema na hatua za kuchukua kwa jamii na wadau mbalimbali utakaowezesha kuandaa wasifu wa maeneo mbalimbali unaoonesha aina ya majanga yanayoweza kutokea katika maeneo hayo.
“Hii itasaidia kuratibu wadau mbalimbali katika utekelezaji wa hatua za kuchukua kufuatia tahadhari za mapema na kuwezesha kufanya maamuzi kabla, wakati na baada ya janga kutokea kwa kushirikiana na vituo vya kisekta katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya ili kuhakikisha vinakuwa na mifumo ya kutoa na kupokea taarifa za majanga mbalimbali inayoendana na mahitaji ya kituo cha Taifa,” amesema
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayemwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), Kamal Kishore, amesema kituo hicho kitashirikiana na vituo vya kikanda na kimataifa vinavyosimamiwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika ili kuboresha udhibiti wa maafa yanayovuka mipaka na Kufuatilia utekelezaji wa taarifa za tahadhari za mapema.
Aidha amesema uharibifu wa mazingira ni chanzo cha majanga mengi ya asili hivyo ni lazima mazingira yatunzwe ili kuepuka majanga hayo ambayo yanasababisha maafa kwa taifa na dunia nzima.
Naye mwakilishi kutoka shirika la hali ya hewa duniani Ernest Afiesimama amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na TMA katika kuhakikisha majanga yote yanachukuliwa tahadhari kabla hayajatokea.
Amesema mpaka sasa shirika hilo limetoa vifaa vya kisasa kwa TMA ambavyo vimeiwezesha mamlaka hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na pia itaendelea kushirikiana nayo ili kukomesha majanga kabla hayaleta madhara kwa wananchi.
Mwisho
Comments
Post a Comment