DK MOLLEL AWASHUKIA WATUMISHI WA UMMA WANAOFUNGIA VITUO VYA KULELEA WATOTO

Muhtasari: Maofisa ustawi wa jamii wametakiwa kuacha tabia ya kuvifungia vituo vya kulelea watoto wanaoishi  kwenye mazingira magumu na hatarishi bila kuwa na mbadala wa mahali pa kuwapeleka watoto hao.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

NAIBU Waziri wa afya, Dk Godwin Mollel amewataka watumishi wa umma kuacha kuvifungia vituo vya kulelea watoto bila kujua watawapeleka wapi watoto hao baada ya vituo hivyo kufungwa.

Dk Mollel ametoa kauli hiyo leo alhamisi Juni 27, 2024 wakati akizungumza  kwenye mkutano Mkuu wa kituo cha kulelea watoto wanaloishi kwenye mazingira magumu na hatarishi Kisedet  kilichopo Kata ya Chigongwe Jijini Dodoma.

Dk Mollel amesema kitendo hicho kinawakatisha tamaa watu ambao wamejitolea kuwalea watoto katika mazingira waliyonayo hivyo badala ya kuvifungia vituo hivyo wanatakiwa waviboreshe ili watoto wasizagae hovyo  mitaani.

"Unakuta mtu ameamua kuwakusanya na kuwalea watoto baada ya kuwaokota huko mitaani anakuja mtumishi wa umma anakifunga hicho kituo kwa madai kuwa hakina sifa, hakuna vitanda vya kuwalaza watoto na mambo mengine, sasa unapokufunga hicho kituo kwa kukosa vitanda vya kuwatosha wakienda huko mitaani ndiyo watapata hivyo vitanda?? unachotakiwa ni kupeleka vitanda na kuboresha mazingira ili watoto wakae eneo salama na si kufunga kituo," amesema Dk Mollel.



Naibu Waziri wa afya Dk Godwin Mollel (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Shirika la Kisedet Jijini Dodoma 


Amesema watu waliojitolea kufungua vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi wanapaswa kupewa ushirikiano na jamii pamoja na serikali kwani wanafanya kazi kubwa ya kulea Taifa la kesho na siyo kwamba wanafanya kazi yenye faida.

Mkurugenzi wa kituo hicho Anderson Ndovu amesema mpaka sasa kituo hicho kimehudumia jumla ya watoto 2,370 ambao wanasoma kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, kuwakutanisha watoto waliokuwa wanaishi mitaani na wazazi wao na kuwapatia ujuzi mbalimbali kupitia vyuo vya kati ikiwemo Veta.

Amesema watoto wengi wanaolelewa kwenye kituo hicho ni wale wanaoishi kwenye mazingira magumu na wengine huwa wanapelekwa kituoni hapo na ofisi za ustawi wa jamii pamoja na polisi baada ya kuwaokota wakiwa hawajui walipotoka au baada ya kutekelekezwa na watu waliowaleta mjini.

"Siku hizi pia tunapokea wasichana wanaofanyakazi za majumbani ambao baada ya kufikishwa mjini waliowaleta waliwafukuza na wakakosa mahali pa kwenda, huwa tunawaunganisha na familia zao," amesema Ndovu.

Amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ni watu kuwapa fedha ambazo huzitumia kununua gundi, kwenda disco, kuchezea kamari na kuwafanya waendelee kubaki mitaani.



Veronica Donald kutoka dawati la jinsia na watoto Wilaya ya Dodoma Mijini akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Shirika la Kisedet Jijini Dodoma


Aidha amelipongeza jeshi la polisi mkoa wa Dodoma kwa kupunguza vifo vya watoto wanaoishi mitaani kwa kushirikiana na vituo vya kulelea watoto hao kwani hali ya Sasa si kama ya zamani.

Naye askari kutoka dawati la jinsia na watoto Veronica Donald amesema kuvunjika kwa ndoa ndiyo sababu kubwa ya watoto kuishi mitaani kwani wazazi wanapotengana watoto hushindwa kupata malezi ya wazazi wote wawili na hivyo kujikuta mitaani wakiomba omba na kuitaka jamii kuboresha Taasisi ya ndoa ili kupunguza wimbi la watoto wa mitaani.

Mwisho...

Comments

Popular posts from this blog

CHODAWU YAITAKA SERIKALI KURIDHIA MKATABA NAMBA 189 WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

NGOs ZAPEWA MWONGOZO WA KULIPA KODI NA TRA

TMDA YATOA MSAADA WA DAWA NA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH 24 MILIONI