WASOMI WA UDOM WATWISHWA JUKUMU LA KUBORESHA MAZINGIRA YA JIJI LA DODOMA

Muhtasari: Wasomi wa chuo kikuu cha Dodoma (Udom) wametakiwa kurejesha uoto wa asili wa Jiji la Dodoma kwa kuanzisha vitalu vya miti ya asili na kuipanda kwenye maeneo ambayo yana uharibifu mkubwa wa mazingira.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

WANAFUNZI wanaosoma chuo kikuu cha Dodoma (Udom) wametakiwa kuanzisha kitalu cha miti ya asili ambayo itapandwa kwenye maeneo yenye uharibifu mkubwa wa mazingira Jijini Dodoma ambao utakuwa mchango wa uwepo wa chuo hicho Jijini humo.

Kauli hiyo imetolewa  na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Lughano Kusiluka kwenye mdahalo wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani uliofanyika chuoni hapo na kuwashirikisha wataalam na wanafunzi wa idara ya mazingira.

Profesa Kusiluka amesema chuo hicho kina wataalam mbali wa masuala ya mazingira hivyo watumie utaalam wao kuhakikisha kuwa Jiji la Dodoma linarejesha uoto wake wa asili ambao umepotea na kusababisha ukame.

“Hii elimu mnayoitoa hapa chuoni tuione ikifanya kazi kwenye mazingira ya nje ya chuo ili tujue kama kweli hii elimu inawasaidia wananchi, anzisheni vitalu vya miti ya asili na mkaipande kwenye makorongo yaliyopo hapa Dodoma huu ndiyo utakuwa mchango wenu kwa Jiji hili,” amesema Prtofesa Kusiluka.

Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi Jiji la Dodoma limekumbwa na ukame ambao umesababisha mvua zikinyesha udongo wote wenye rutuba unachukuliwa na maji na hivyo kutengeneza makorongo makubwa yanayohatarisha makazi ya watu.

“Tunataka tuone Udom inapanda miti kwenye makorongo yote yaliyopo hapa na tutakapoiona miti imestawi na makorongo yamepotea ndipo tutajua umuhimu wenu hapa naamini serikali ikiona juhudi zenu haitaacha kushirikiana na nyinyi,” amesema Profesa kusiluka.

Kwa upande wake mkuu wa idara ya Jiografia na stadi za mazingira wa Udom Profesa Ebiudi Kaswamile amesema mikoa inayoongoza kwa uharibifu wa mazingira nchini  ni Dodoma, Singida, Tabora,  Shinyanga na Lindi huku mikoa ambayo inajitahidi kuyatunza mazingira ni Kagera, Mara, Kigoma, Katavi, Rukwa na Njombe.

Amesema serikali na wadau wana wajibu wa kutoa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira ili kuiepesha nchi na janga la ukame na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kila mtu ameyaona kwa siku za hivi karibuni.

Wakichangia maoni yao kwenye mdahalo huo wanafunzi wa chuo hicho wameliomba Baraza la usimamizi wa mazingira nchini (NEMC) kuwashirikisha vijana wasomi kwenye kada ya mazingira kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira hasa maeneo ya vijijini ambako ndipo kuna watu wengi wanaolima na kutumia nishati ya kuni na mkaa.

Jacklina Innocent amesema serikali iwatumie vijana wenye ujuzi na masuala ya mazingira katika kuyatunza kwani wengi wamesomea kada hiyo lakini wapo mitaani hawana ajira na wakati shughuli za kufanya zipo.

Mwisho…

Comments